Melbourne, Australia
Mechi ya mahasimu wa Ligi A nchini Australia, Melbourne City na Melbourne Victory ililazimika kusimamishwa juzi jioni baada ya kipa wa Melbourne City, Tom Clover kuumizwa usoni baada ya mashabiki kuvamia uwanjani.
Tukio hilo lilitokea dakika ya 22 ya mchezo huo ambapo kipa huyo mwenye miaka 24 inaaminika aliumizwa na kitu cha bati usoni na kutokwa na damu hapo hapo baada ya kundi kubwa la mashabiki kuvamia uwanja na huku wengine wakirusha fataki.
Mbali na kipa, mwamuzi wa mchezo huo, Alex King naye alijeruhiwa na mashabiki ingawa Chama cha Soka Australia hakijaeleza kwa undani ukubwa wa majeraha aliyopata mwamuzi huyo.
Hatimaye mechi hiyo ilifutwa kwa usalama wa wachezaji huku sababu hasa za vurugu hizo ikielezwa kuwa ni mashabiki kutokubaliana na uamuzi wa bodi ya ligi kuuza haki za mechi hiyo kwa miaka mitatu ijayo jambo lililowakera mashabiki hao ambao waliingia uwanjani na mabango ya kupinga uamuzi huo.

Wakati tukio hilo linatokea City walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0 ambapo kundi kubwa la mashabiki lilivamia uwanjani na katika kipindi hicho ndipo kipa na mwamuzi walipojeruhiwa huku eneo hilo likiwa limetanda moshi uliotokana na fataki zilizokuwa zikilipuliwa na mashabiki.
Baada ya hali kuonekana kuwa mbaya, wachezaji akiwamo nyota wa zamani wa Ureno na Man United, Nani walitolewa kwenye eneo la uwanja kwa ajili ya usalama wao.
Taarifa ya Chama cha Soka Australia baadaye ilieleza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika wa vurugu hizo na tayari uchunguzi kwa lengo la kubaini chanzo na wahusika umeshaanza kufanyika mara moja.
