Manchester, England
Beki wa Man United, Harry Maguire ambaye amekuwa akihaha kupata namba, amesema uamuzi wake wa kubaki katika klabu hiyo majira ya kiangazi umempa ushindi baada ya kurejea kikosi cha kwanza.
Baada ya kuwa na wakati mgumu katika msimu wa kwanza chini ya kocha Erik ten Hag, Maguire alikuwa mbioni kujiunga na West Ham wakati wa dirisha la usajili lakini mwishowe aliamua kubaki Man United.
Msimu huu wa 2023-24 aliuanza akiwa benchi lakini katika mechi nane za michuano yote zilizopita, mchezaji huyo amekuwa akipata nafasi kikosi cha kwanza na hivyo anaamini alikuwa sahihi kuamua kubaki Man United.
“Nilicheza mechi chache mno msimu uliopita, 16 au 17 kwenye kikosi cha kwanza na nadhani nilicheza vizuri katika mechi nilizopata nafasi, japo sikucheza mechi nyingi kama ambavyo ningependa,” alisema Maguire.
“Nililazimika kuwa mvumilivu, nilipata nafasi mbili au tatu za kucheza msimu uliopita lakini nikajikuta katika majeruhi mara mbili, kwa hiyo sikuwa kwenye ile kasi na sikupata mechi mfululizo za kutosha ambazo ningeweza kuzitumia kumthibitishia kocha, nimepata nafasi hiyo sasa,” alisema Maguire.
“Hakika nafurahia soka langu na nafurahia hasa kuichezea hii klabu, nilikuwa tayari kubaki hapa na kupigania nafasi yangu na hapa tuna mabeki wa kati wenye hadhi ya kimataifa wanne au watano, ukweli ni kwamba ushindani wa namba ni mkubwa mno,” alisema Maguire.
Maguire kwa sasa ndiye beki wa bei mbaya zaidi duniani akiwa amesajiliwa Man United mwaka 2019 kutoka Leicester City kwa ada ya Pauni 80, na sasa ameanza kupata nafasi kikosi cha kwanza baada ya Martinez kuwa majeruhi wa muda mrefu.