London, England
Kiungo wa zamani wa Man Utd, Roy Keane amesema ataendelea kumtetea nyota wa timu hiyo, Cristiano Ronaldo wakati winga wa zamani wa Liverpool, Jermain Pennant akidai kwamba alichofanya mchezaji huyo ni kitu cha hovyo.
Ronaldo alisusa kuingia uwanjani katika mechi na Tottenham Jumatano iliyopita na kutoka dakika chache kabla ya mpira kumalizika wakati timu yake ikiongoza kwa mabao 2-0 jambo lililomkera kocha wa timu hiyo, Eric ten Hag ambaye aliahidi kumchukulia na alianza kwa kumuondoa katika kikosi cha timu hiyo ambacho jana Jumamosi kiliumana na Chelsea na kutoka sare ya bao 1-1.
Akimtetea mchezaji huyo Keane alisema kuna wachezaji ambao wamekuwa wakifanya mambo mabaya kuliko hilo na kuitaja tabia hiyo kuwa ni kama hulka ya kibinadamu kwa wachezaji na alichofanya Ronaldo ni kuonyesha jinsi anavyoijali klabu.
“Mimi hata hivyo naliangalia hili katika mtazamo wa mchezaji, ni wazi kwamba amechoka, amevurugwa kichwani na nafikiri tatizo lilikuwa linamsumbua kwa wiki kadhaa na akachoka na kuamua kutoka uwanjani,” alisema Keane.
Akifafanua hoja yake ya kwamba Ronaldo ni mchezaji anayejali Keane alisema, “ningekuwa na wasiwasi zaidi kama Ronaldo angekuwa anakaa benchi kila wiki huku akicheka na kutojali hali hiyo na ndio maana mimi nafikiri jamaa anajali.”
“Kuna watu wanasema Ronaldo huyu si tena yule mchezaji waliyekuwa naye miaka 10 iliyopita, ni kweli si yule lakini msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa Man United, alijiunga na Man United mwaka jana, Man United mbaya, mbaya hasa lakini bado akawa mfungaji bora.

Wakati Keane akiwa na mtazamo huo, Pennant ambaye mbali na Liverpool pia amewahi kuichezea Arsenal aliponda kitendo cha mchezaji huyo kujisafisha kupitia mtandao wa Instagram akidai kwamba alichofanya ni kitu cha hovyo na ni kielelezo cha ubinafsi.
“Ni kitu cha hovyo, mwishowe unatakiwa kuwa na ubinadamu na kukubali kosa lako, simama na useme jamani nimelikoroga na naomba msamaha, kwanza kwa wachezaji wenzangu, kocha wangu, klabu na mashabiki,” alisema Pennant.
“Taarifa aliyoitoa haionyeshi kubeba msalaba wa kosa lake, hakuna kuomba msamaha, ni kujiangalia binafsi, na jinsi nilivyofanya hivyo na vile, ni upuuzi mtupu, ni kama kujijenga yeye na si kile ambacho alitakiwa kukifanya,” aliongeza Pennant.
Naye mshambuliaji wa zamani wa England, Darren Bent alikubaliana na Pennant na kuongeza kuwa Ronaldo amefanya dhihaka kwa kusema kwamba atakuwa mfano mzuri kwa wachezaji chipukizi tangu arudi katika klabu hiyo miezi takriban 12 iliyopita.
“Tunajua alivyokuwa mchezaji mzuri, ni mmoja wa wachezaji wakubwa kuwahi kutokea, lakini tunazungumzia ya wakati huu, na yanayoendelea sasa,” aliongeza Bent.
