Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza amesema hana mpango wa kushindana na mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele kuwania kiatu cha ufungaji bora msimu huu kwa kuwa amewekeza nguvu kubwa kuisaidia timu kwanza.
Ntibazonkiza alifunga mabao matano jana katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na hivyo kufikisha mabao 15 nyuma ya Mayele aliyefunga mara 16.
Ntibazonkiza hata hivyo alisema anashukuru kuisaidia timu yake kupata matokeo na kama itatokea atatwaa kiatu cha ufungaji bora basi itakuwa vizuri lakini kwa sasa anaitanguliza Simba kisha mambo mengine yatafuata.
“Kwa sasa ni timu kwanza kupata matokeo mazuri kisha vingine hivyo tutaangalia kitakachotokea kwa uwezo wa Mungu. Fiston ni mfungaji mzuri, mshambuliaji mzuri kila mtu anamjua kwa hiyo ikitokea nikifanikiwa kuchukua nitamshukuru Mungu lakini timu kwanza,” alisema Ntibazonkiza.
Kwa mabao matano aliyofunga juzi, Ntibazonkiza anakuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga mabao mengi katika mechi moja lakini pia akifunga ‘hat-trick’ya pili msimu huu, sawa na nahodha wa Simba, John Bocco.
