London, England
Kocha wa muda wa Chelsea Frank Lampard amesema hatarajii kumaliza matatizo ya timu hiyo kwa siku moja baada ya kufungwa bao 1-0 na Wolves jana Jumamosi katika mechi yake ya kwanza tangu akabidhiwe timu hiyo.
Lampard, kocha, nahodha na mchezaji wa zamani wa Chelsea, hivi karibuni alikabidhiwa jukumu zito la kuinoa timu hiyo inayosuasa katika Ligi Kuu England (EPL) baada ya kutimuliwa kwa Graham Potter.
Hii ni mechi ya nne kwa Chelsea kushindwa kupata ushindi ikiwa inashika nafasi ya 11 kwenye EPL msimu huu na tayari imeanza kupoteza matumaini ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
“Ni jukumu zito kuiongoza Chelsea, tunajua tuko katika nafasi ambayo hatutaki tuwe nafasi hiyo, wakati wote huwa kuna sababu katika hilo,” alisema Lampard.
“Sikutarajia kuweka kila kitu sawa kwa siku moja, ni lazima muwe washindani katika mechi zenu, kasi zaidi na ushindani zaidi,” alisema Lampard ambaye hivi karibuni alifutwa kazi Everton.
“Wachezaji wanatakiwa kulielewa hilo kwa sababu bila ya hivyo huwezi kushinda mechi, hata hivyo ni jambo zuri niko hapa kusaidia katika hilo na si kukutana na shutuma kali, najua vipo vipaji vingi,” alisema.
Jumatano ijayo Chelsea itakuwa na kibarua kizito ugenini katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya mabingwa watetezi wa taji hilo, Real Madrid.
“Nina furaha kurudi hapa, tuna mechi kubwa inatusubiri Jumatano, mechi ambayo kila kitu kitabadilika,” alisema akiizungumzia mechi yao na Real Madrid.
Alipoulizwa kuhusu ukubwa ya jukumu linalowakabili wachezaji wake dhidi ya Real Madrid, Lampard alisema, “Kama una hofu huna sababu ya kuja, sisemi kwamba kikosi hakina upambanaji bali ni suala ya kuweka mambo pamoja, mechi ya Jumatano itakuwa tofauti kabisa.”
Lampard ametua Chelsea akitokea Everton alipotimuliwa Januari mwaka huu, kabla ya hapo aliinoa Chelsea kuanzia Julai 2019 kabla ya kutimuliwa Januari 2021.
Mwaka 2012 Lampard alikuwa mchezaji wakati Chelsea ikitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, timu hiyo ilikuwa ikinolewa na kocha wa muda, mtaliano Roberto di Matteo.