Na mwandishi wetu
Uongozi wa Yanga, upo katika hatua za mwisho kumtangaza kiungo wa Ivory Coast na Asec Mimosas, Pacome Zouzoua kusajiliwa na timu hiyo akitajwa kuwa mrithi sahihi wa Fiston Mayele.
Mayele, mshambuliaji nyota na kinara wa mabao katika Ligi Kuu NBC, ameuzwa katika klabu ya Pyramids ya Misri kwa Sh bilioni 2 na nafasi yake imekuwa mjadala kwa siku kadhaa sasa.
Baada ya usiku wa kuamkia juzi, timu hiyo kumtambulisha Mahlatsi Makudubela ‘Skudu’ kutoka Marumo Gallants, uongozi wa Yanga umepanga kufunga pazia la usajili kwa kumtangaza Zouzoua anayemudu vyema eneo la ushambuliaji.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alisema walikuwa na machaguo mengi, lakini kocha wao mkuu, Miguel Gamondi amevutiwa na Zouzoua ambaye baada ya kumfuatilia ameona kuwa ni mbadala sahihi wa Mayele.
“Kocha amevutiwa na Zouzoua sababu zake ni kwamba yupo mchezoni si kama hao wengine ambao tunaambiwa walikuwa nje lakini kingine alichosema ni mshambuliaji huyo ana uwezo mkubwa wa kufunga kama alivyokuwa Mayele vitu ambavyo vimemvutia,” alisema Kamwe.
Alibainisha kuwa tayari walishaanza mchakato wa kumsaka mchezaji huyo na kama mambo yakienda sawa wanatarajia kumtambulisha ili aweze kushiriki kwenye mchezo wao wa kilele cha Wiki ya Mwananchi, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kamwe pia alisema wageni wao kuelekea mchezo wao wa kirafiki wa Jumamosi, timu ya Kaizer Chiefs inatarajia kutua nchini kesho Alhamisi ikiwa na kikosi chake kamili kwa ajili ya mchezo huo utakaosherehesha Wiki ya Mwananchi.
Alisema mpaka sasa maandalizi yote kuelekea tamasha hilo yanakwenda vizuri na sherehe zao zinatarajiwa kuhudhuriwa na watu mbalimbali ikiwemo idadi kubwa ya wasanii wa tasnia zote nchini.