Manchester, England
Kiungo Bruno Fernandes ametangazwa kuwa nahodha mpya Man United akichukua nafasi ya Harry Maguire aliyevuliwa jukumu hilo na kocha Erik ten Hag baada ya kukosa namba ya uhakika kikosi cha kwanza.
Fernandes (pichani) amekabidhiwa jukumu hilo akiwa na rekodi ya kuichezea timu hiyo mechi 185 na kufunga mabao 64 akiwa pia na asisti 54 katika mashindano yote.
Kiungo huyo tayari alianza kutekeleza majukumu ya unahodha kwa muda mrefu kwenye msimu uliopita wa 2023-34 pale Maguire alipokosekana kwenye timu kwa kuwa majeruhi au kukosa namba.
Man United bado haijawa tayari kupokea ofa ya Maguire ambaye West Ham United iliwahi kumuulizia katika dirisha dogo la usajili la Januari lakini mabosi United hawakulipa umuhimu suala hilo.
“Kiungo huyu wa Ureno tayari ameshawahi kuvaa kitambaa cha unahodha cha United katika mechi kadhaa na Erik ten Hag amethibitisha kwamba sasa mchezaji huyo ataendelea na jukumu hilo moja kwa moja,” ilisema taarifa ya Man United.
Katika moja ya matukio mabaya ya kukumbukwa ya Fernandes ni siku ambayo Man United ililala mbele ya Liverpool kwa mabao 7-0 katika msimu uliopita wa 2022-23 na mchezaji huyo kulaumiwa kwa kucheza chini ya kiwango.