Dubai, UAE
Kiungo fundi wa zamani wa Barcelona na timu ya Taifa ya Hispania, Andres Iniesta, 39, amejiunga na klabu ya Emirates ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Iniesta amewasili Dubai jana Jumatatu kusaini mkataba ambao pia una kipengele kinachompa nafasi ya kuongeza mwaka mwingine mmoja na hivyo anaweza kucheza na klabu hiyo hadi mwaka 2025.
Hatua ya mchezaji huyo kuelekea UAE, ni hatua nyingine ya kuendelea kucheza soka nje ya Barca kwani katika misimu mitano iliyopita alikuwa Japan akiichezea klabu ya Vissel Kobe na ameondoka akiwa amemaliza mkataba na klabu hiyo.
Akiwa na Kobe, Iniesta alicheza kwa dakika 94 katika jumla ya mechi 18 za timu hiyo msimu uliopita lakini anaonekana mwenye matamanio ya kuendelea kucheza soka licha ya umri kuwa mkubwa.
“Nimejifunza mengi katika miaka hii mitano ambayo ni mingi, kulikuwa na ugumu pale ambapo hupewi nafasi ya kucheza baada ya kuweka moyo wangu kwenye mazoezi,” alisema Iniesta mwezi uliopita baada ya kucheza mechi ya mwisho akiwa na Kobe.
Iniesta anakumbukwa kwa kuwa kiungo muhimu ambaye ndiye aliyefunga bao la ushindi lililoipa Hispania Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, na alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu walioiwezesha Barca kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008 na 2012.
Alianza kucheza soka la ushindani Barca ambapo pia amebeba mataji tisa ya La Liga, manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mataji mengine kadhaa katika misimu 16 aliyokuwa na timu hiyo.
