Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumamosi imeichapa Al Merrikh ya Sudan bao 1-0 na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo baada ya miaka takriban 25.
Clement Mzize ndiye aliyeifungia Yanga bao pekee katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Azam Complex na kuifanya timu hiyo isonge mbele kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza.
Mzize ambaye aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Kennedy Musonda na kufunga bao hilo pekee kwa kichwa akiunganisha krosi iliyopigwa na Joyce Lomalisa.
Kasi ya Mzize kusaka bao ilianza kuonekana dakika mbili tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili alipounganisha kwa kichwa krosi ya Maxi Nzengeli na mpira kujaa wavuni lakini bao hilo lilikataliwa kwa kuwa krosi ya Nzengeli ilipigwa mpira ukiwa umetoka.
Merrikh ilionekana waliingia na mpango mzuri wa kulinda wasifungwe na Yanga na kutafuta bao la kushtukiza kwa namna walivyojitahidi kuvuruga mipango ya Yanga hasa kwa kumdhibiti Stephane Aziz Ki ambaye baadaye alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Pacome Zouazoua.
Aziz Ki pamoja na kubanwa lakini hakukosa nafasi ya kuonesha ubora wake wa kufumua mashuti ambapo mashabiki wa Yanga waliinuliwa vitini na shuti la mchezaji huyo ambalo hata hivyo liligonga mwamba na kurejea uwanjani hilo likiwa shambulizi pekee kali la mchezaji huyo kabla ya kutolewa.
Merrikh kwa upande wao walikuwa na wakati mgumu kuipenya ngome ya Yanga hasa beki ya kulia iliyolindwa vyema na Kwasi Yao ambaye alikuwa mahiri kwa kipindi kirefu cha mchezo huo.
Kwa ushindi huo Yanga sasa inasubiri kuwajua wapinzani wake katika hatua ya makundi baada ya makundi hayo kupangwa baadaye mwezi Oktoba na mechi zake kuanza kuchezwa Novemba.
Baadhi ya timu ambazo tayari zimefuzu hatua hiyo na huenda zikapangwa kundi moja na Yanga ni pamoja na Mamelodi Sundowns, TP Mazembe, Al Alhly na Pyramids za Misri na Perto Atletico ya Angola.
Kimataifa Yanga yafuzu makundi Afrika
Yanga yafuzu makundi Afrika
Read also