Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa timu za soka za Taifa za Wanawake, Bakari Shime (pichani) amesema walifanikiwa kuichapa Burundi mabao 3-0 kutokana na kubadili mipango kwenye kipindi cha pili cha mechi hiyo.
Shime alisema hayo baada ya mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa timu za wanawake chini ya miaka 18 yanayofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
“Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri na wachezaji hawakucheza kwenye maelekezo na muda mrefu walipambana kutafuta bao. Kipindi cha pili walirudi kwenye mtindo wetu, tukatengeneza nafasi na kumiliki mpira mwishoni tukapata matokeo tuliyotarajia,” alisema Shime.
Kuhusu mchezo wa kesho Alhamisi dhidi ya Ethiopia, Shime alisema lengo lao ni kuhakikisha wanachukua ubingwa hivyo ushindi ni muhimu katika kila mchezo.
Mashindano hayo yanachezwa kwa mtindo wa ligi na yanashirikisha timu tano ambazo ni Tanzania, Burundi, Uganda, Ethiopia na Zanzibar huku Rwanda na Kenya zikiwa zimejitoa.
Mchezo mwingine uliopigwa jana ulizikutanisha Uganda na Ethiopia ambapo Uganda ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.