London, England
Mfanyabiashara wa Finland, Thomas Zilliacus ametangaza nia ya kuinunua klabu ya Manchester United, siku chache baada ya Sheikh Jassim bin Hamad Al-Thani wa Qatar naye kudaiwa kuitaka klabu hiyo.
Zilliacus, mmiliki wa kampuni ya habari ya mitandao ya kijamii anataka kununua nusu ya klabu hiyo na nusu nyingine inunuliwe na mashabiki ambao watahusika katika maamuzi mbalimbali ya uendeshaji.
Awali watu wote waliokuwa na nia ya kununua hisa nyingi katika klabu hiyo walitakiwa kuwasilisha rasmi maombi yao hadi juzi Jumatano kabla ya muda huo kuongezwa.
“Klabu yoyote ya michezo mwisho wa siku ni mali ya mashabiki, maombi yangu ya kuinunua klabu yanajengwa na usawa kwa mashabiki,” alisema Zilliacus.
“Mipango ya maendeleo ya klabu iliyopo sasa ambapo masheikh mabilionea na watu wao wanamiliki klabu na kuzisimamia kama mali zao si utaratibu ‘wenye afya’,” aliongeza Zilliacus.
“Thamani ya klabu kwenye soko kwa sasa ni chini ya Dola 3.9 bilioni, maana yake ni kwamba kama mashabiki watahusika kuinunua klabu, kila shabiki atatakiwa kutoa si zaidi ya dola 6 tu,” alisema Zilliacus.
“Kampuni yangu itatoa nusu iliyobaki ili kuimiliki klabu na tutawataka mashabiki kupitia kampuni mpya ambayo itaundwa wawe wahusika, wakihusika wote inaweza kuwa chini ya dola 3 kwa kila shabiki,” aliongeza Zilliacus.
Katika mipango yake ya uendeshaji klabu, Zilliacus atawaandalia mashabiki mtandao maalum wawe wanashiriki kupiga kura na kutoa maoni wanapotaka kuamua jambo kuhusu soka katika klabu yao.
Zilliacus ambaye si mtu kwenye michezo akiwa amehusika zaidi katika mchezo wa ‘ice hockey’ kwao Finland ni mwenyekiti na mwanzilishi wa kampuni ya habari mitandao ya novaM.
Mbali na Zilliacus na Sheikh Jassim ambao wametangaza nia zao hadharani, tajiri mwingine anayeitaka Manchester United ni Sir Jim Ratcliffe. Klabu hiyo kwa sasa inamilikiwa na familia ya Glazer.