Doha, Qatar
Nahodha wa timu ya Taifa ya Wales, Gareth Bale amefuta madai ya kwamba anastaafu kuichezea timu yake ya taifa badala yake amesema yuko tayari kuendelea kuichezea timu hiyo iwapo atahitajika kufanya hivyo.
Kauli ya Bale imekuja baada ya uvumi kwamba nyota huyo wa zamani wa Real Madrid na Tottenham ambaye kwa sasa ana miaka 33, angestaafu mara baada ya fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zinazoendelea Qatar.
Wales, jana Jumanne ilichezea kipigo cha mabao 3-0 mbele ya England katika mechi ya Kundi B, matokeo ambayo yameifanya ishike mkia katika kundi lake na kuaga rasmi fainali hizo.
Bale, ambaye kwa sasa anacheza soka nchini Marekani hata hivyo amesema kwamba atarudi kushiriki mechi za kimataifa za Wales wakati kocha wa timu hiyo, Robert Page atakapoanza mbio za kuwania kufuzu fainali za Euro 2024, mwezi Machi mwakani.
“Nitaendelea kupambana kadri niwezavyo iwapo nitahitajika, tuko katika kipindi kigumu kwa sasa lakini tunaendelea kupambana, tuna kampeni za kuwania kufuzu Euro Machi mwakani, tuna miezi michache imebaki, kabla ya kuingia kwenye soka la kimataifa, inasikitisha kwa sababu tulipenda kubaki kwenye Kombe la Dunia kwa muda mrefu, lakini tuna kazi mwezi Machi,” alisema Bale.
Katika mechi na England, Bale alitolewa wakati wa mapumziko na nafasi yake kuingia Brennan Johnson na baadaye alisema kwamba alianza kusikia maumivu ya misuli kabla ya mechi kuanza na hivyo angekuwa mbinafsi kuendelea kucheza wakati hakuwa na uwezo wa kukimbia.
Matokeo Kombe la Dunia…
Ecuador 1-2 Senegal
Uholanzi 2-0 Qatar
Wales 0-3 England
Iran 0-1 Marekani
