London, England
Kitendo cha kipa mpya wa Man United, Andre Onana (pichani) kumkaripia beki Harry Maguire kimemkera mshambulijai wa zamani wa Aston Villa, Gabby Agbonlahor ambaye amesema haoni kosa la Maguirre.
Onana alimjia juu Maguire katika mechi ya kirafiki iliyopigwa mjini Las Vegas jana Jumatatu dhidi ya Borussia Dortmund, mechi ambayo Man United ililala kwa mabao 3-2.
Kipa huyo aliyesajiliwa kwa ada ya Pauni 47 milioni kutoka Inter Milan ya Italia, aliingia kipindi cha pili, alimjia juu Maguire akimlaumu kwa kutoa pasi dhaifu kwa Christian Eriksen iliyokuwa sababu ya Dortmund kuupata mpira.
Baada ya mpira kutoka, Onana alianza kumkaripia Maguire pembeni ya eneo la penalti huku akionesha dalili zote za kuwa mwenye hasira japo haikueleweka alichosema lakini tukio hilo limemkera Agbonlahor ambaye amesema kwamba Onana hakuwa na sababu ya kufanya alichofanya.
“Awali ya yote Harry Maguire hakufanya kosa lolote, alitoa pasi kwa mchezaji wa kiungo ambaye ndiye aliyeupoteza mpira na naona kama Maguire ni mtu ambaye amekuwa rahisi kushambuliwa,” alisema Agbonlahor.
“Sijapenda kilichofanywa na Onana, naona Maguire ni mtu ambaye amekuwa rahisi kushambuliwa, je unaweza kufanya hivyo kwa Martinez? sidhani kama inawezekana? Au kufanya hivyo kwa Rashord?,” alisema Agbonlahor.