Na mwandishi wetu
Kila mchezaji ana nafasi yake katika mechi ya Simba na Yanga inayopigwa jioni ya leo, kwa Fiston Mayele, mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona kama atatema au la.
Yanga na Simba zinaumana jioni ya leo kwenye Uwanja wa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Azam, mechi ambayo kwa Mayele suala la kutupia na kutetema ni kitu kinachosubiriwa na mashabiki wa Yanga wakati wale wa Simba shauku yao ni kuona anavyodhibitiwa kama ilivyokuwa katika mechi mbili zilizopita.
Mechi ya leo inakuwa ya tatu katika msimu mmoja, katika mechi mbili zilizopita ambazo ni za Ligi Kuu ya NBC Bara, zote zilitawaliwa na matokeo ya bila kufungana hivyo matokeo ya leo yatakuwa na maana kubwa kwa mshindi.
Kwanza timu itakayoshinda itakuwa imejikatia tiketi ya kucheza fainali dhidi ya mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Coastal Union na Azam itakayochezwa kesho, pili mshindi atakuwa na kila sababu ya kujivania kwa kumaliza msimu akiwa mbabe baada ya mechi mbili za sare.
Mayele mshambuliaji kinara wa mabao Ligi Kuu ya NBC akiwa na mabao 14 sawa na George Mpole wa Geita Gold, mechi hiyo inaendelea kuwa na maana kubwa kwake, kwanza atataka kuifunga Simba baada ya kuikosa katika mechi mbili za ligi lakini pia ukubwa wa mechi hiyo na ushindani wa jadi uliopo ni mambo ambayo yanafanya bao la mchezaji huyo kuwa na maana kubwa.
Ni bao ambalo hapana shaka litaandamana na mitetemo yake iliyozoeleka lakini pia litakuwa kama limeamsha kasi yake ya mabao ambayo imekuwa ya kusuasua katika mechi za hivi karibuni za Yanga.
Kwa Mayele hata hivyo suala la kutetema ni jambo rahisi hasa pale unapouzungumzia ukuta wa Simba hasa eneo la kati ambalo linadhibitiwa vizuri na watu wawili wanaojua wajibu wao, Mkenya Joash Onyango na Mkongomani, Henock Inonga.
Kwa mashabiki walio wengi vita ya wababe hao ilianza kuonekana Desemba mwaka jana timu hizo zilipokutana katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC, dakika ya 20 tu Mayele aliunganishiwa pande na kupambana na Onyango ambaye alimzidi ujanja na kuondoa hatari golini.
Dakika kama tano baadaye, Mayele aliunasa mpira akaupenyeza katikati ya miguu ya Onyango ambaye kama si akili yake ya ziada ya kumzibia njia, Mayele angetetema, kwa kumzuia huko Onyango akalimwa kadi ya njano na Yanga kupewa mpira wa adhabu.
Dakika 10 baadaye wawili hao walikutana safari hii wakiwania mpira wa juu ambao alipasiwa Mayele lakini wakiwa katika mbio hizo, Onyango alimpa Mayele mwili na kwa kuwa Mayele alikuwa kwenye kasi akashindwa kufanya alichotaka kufanya.
Dakika tatu kabla ya mapumziko, Mayele aliunganishiwa tena mpira wa juu ambao kipa wa Simba, Aishi Manula aliufuata lakini alishindwa kuudaka baada ya kuteleza na hivyo kumpa Mayele nafasi ya kuuwahi huku akifukuziwa kwa karibu na Onyango lakini akiwa ameshauzuia mpira Mayele naye akateleza na hapo ikawa rahisi kwa Onyango kuondoa hatari.
Hatimaye mabosi benchi la ufundi Yanga wakaamua kumtoa Mayele katika dakika ya 82 na hapo ndipo alipoibuka Inonga akionekana kumsindikiza Mayele nje ikiwa ni kama vile kuashiria kwamba wamefanikiwa kudhibiti mitetemo ya mchezaji huyo.
Vita ya Desemba ikaishia hapo, Aprili 30 mwaka huu timu hizo zilipokutana tena, Mayele akaendelea kuwa gumzo lakini hakuweza kutetema na safari hii kazi kubwa ilifanywa na Inonga.
Safari hii mpambano ulianzia dakika ya 15, Mayele aliunganishwia pasi na Djuma Shaban lakini wakati akielekea kumkabilia kipa Aishi Manula, Inonga aliusotea mpira kwa chini na kuuwahi akaondoa hatari huku akionyesha mikono juu kuashiria alivyomdhibiti Mayele.
Dakika nane baadaye pasi ya upande wa kulia iliwakutanisha wawili hao lakini tena alikuwa ni Inonga aliyeuwahi mpira na kumuacha Mayele akiwa hana la kufanya.
Mayele alidhibitiwa tena dakika ya 32 safari hii kazi kubwa ikifanywa na Onyango ambaye baada ya kuuwahi mpira ilibidi autoe nje. Dakika 10 baada ya mapumziko, Mayele na Inonga walipambana tena kuwania mpira ambao Inonga kwa mara nyingine alilala chini na kuuwahi na kufanikiwa kuondoa hatari langoni mwake.
Yote hayo yanabaki kuwa historia swali moja linabaki je Mayele baada ya kushindwa kutupia na kutetema mara mbili kwenye dimba la Kwa Mkapa, ataweza leo kwenye dimba la Kirumba? Tusubiri.
