Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya KMC, umesema hauna mpango wa kumwachia kocha wao mkuu, Abdulhamid Moallin ambaye inaelezwa kuwa anahitajika na timu yake ya zamani ya Azam FC.
Akizungumza na GreenSports, Meneja Habari na Mawasiliano wa KMC, Khalid Chukuchuku alisema wana malengo makubwa na kocha huyo hasa kutokana na programu aliyoianzisha ya kuijenga timu yao na kuirudisha kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao.
“Hatuna mpango wa kuachana na kocha wetu Moalin, tuna mkataba naye wa muda mrefu lakini mpaka sasa tunaridhishwa na mwenendo wa timu yetu tangu kuanza kwa msimu huu kwani katika michezo tisa tumepoteza miwili na tupo kwenye nne bora, hii ni tofauti na tulivyokuwa msimu uliopita,” alisema Chukuchuku.
Meneja huyo alisema hata wao wamekuwa wakizisikia taarifa za kocha wao kuhitajika Azam lakini hawatokubali hilo litokee kwani wanaridhishwa na kile ambacho anakifanya kwenye timu yao tangu wamemuajiri mwanzoni mwa msimu huu.
Hivi karibuni kumeibuka fununu za Azam yenye maskani yake Chamazi, Dar es Salaam ikidaiwa kuhitaji huduma ya Moallin kwa ajili ya kwenda kuongeza kitu kuiweka sawa timu hiyo ambayo msimu huu imekuwa haina mtiririko wa matokeo mazuri.
Katika hatua nyingine, Chukuchuku alozungumzia kipigo walichokipata juzi dhidi ya Dodoma Jiji FC ambapo alikubali matokeo na kueleza kuwa wanajipanga kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mechi zinazofuata za ligi.
Alisema malengo yao msimu huu ni kumaliza ligi ndani ya tano bora lakini kwa mzunguko wa kwanza ni kuhakikisha wanamaliza ndani ya tatu bora na hadi sasa wapo ndani ya malengo yao kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.
