Madrid, Hispania
Kocha mpya wa Real Madrid, Xabi Alonso amemaliza mazoezi yake ya kwanza akiwa na timu hiyo jana Jumatatu huku akipewa angalizo na rais wa klabu hiyo, Florentino Pérez.
Katika angalizo lake Perez alimtaka kocha huyo kutambua umuhimu wa mashindano ya Fifa ya Kombe la Dunia la Klabu yanayotarajia kuanza kutimua vumbi baadaye mwezi huu.
Alonso, kocha wa zamani wa Bayer Leverkusen ambaye amechukua nafasi ya Carlo Ancelotti mwezi uliopita, alianza kazi hiyo kwenye uwanja wa mazoezi wa timu hiyo wa Valdebebas akiwa na wachezaji wachache wa kikosi cha kwanza.
Baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho wapo kwenye timu zao za taifa na wengine majeruhi hivyo baadhi ya wachezaji wa akiba waliongezwa ili kuongeza idadi ya wachezaji kwenye mazoezi hayo.
Real Madrid imebakiwa na siku nne za kufanya mazoezi kabla ya kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya mashindano hayo yanayoandaliwa na Fifa.
Baada ya kuwa katika msimu mgumu wa 2024-25 uliomalizika hivi karibuni na kushindwa kubeba taji la La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na lile la Mfalme ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2021, Perez anaamini timu hiyo inaweza kushinda taji la Klabu la Dunia.
“Mnajua kwamba katika klabu hii wakati wote huwa tunahitaji zaidi, na kwa sasa tuna furaha kubwa kuwamo kwenye Kombe la Dunia la Klabu, michuano inayofanyika Marekani,” alisema Perez.
Perez alisema kwamba anaamini wachezaji wa timu hiyo watajitoa kwa uwezo wao wote ili kuhakikisha wanashinda taji hilo.
