Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema kikosi chake kipo tayari kuikabili Wydad Casablanca na kupata ushindi bila kuhofia ubora wa wapinzani wao hao.
Simba Jumamosi hii itashuka kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kukabiliana na Wydad ikiwa ni mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Robertinho ameeleza kuwa walishakamilisha maandalizi ya mchezo huo siku nyingi, wanachokifanya sasa ni kupeana vitu vidogo vidogo ikiwemo mbinu muhimu zitakazowawezesha kupata ushindi.
“Tupo tayari kwa mchezo na ninaamini tutashinda, sababu wachezaji wangu wana ari kubwa ya kupambana, najua ni mchezo mgumu kutokana na ubora waliokuwa nao wapinzani lakini tupo tayari kwa mapambano lengo ni kupata ushindi,” alisema Robertinho.
Kocha huyo ameeleza kuwa anaipa Simba nafasi kubwa ya kusonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali kutokana na mikakati ambayo timu yake imeiweka kwenye michuano hiyo hivyo haoni sababu ya mashabiki wao kuwa na hofu.
Wapinzani wa Simba, Wydad Casablanca wanatarajiwa kuwasili nchini kesho Alhamisi wakiwa na msafara wa watu 50 ambao ni wachezaji pamoja na viongozi mbalimbali wa timu hiyo.