Madrid, Hispania
Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Hispania (RFEF) Luis Rubiales anayekabiliwa na kashfa ya kumbusu mdomoni mchezaji wa timu ya taifa, amekamatwa kwa ajili ya uchunguzi unaomhusisha na kashfa ya kupokea rushwa.
Rubiales alikamatwa jana Jumatano mara baada ya kuwasili jijini Madrid akitokea Jamhuri ya Dominica ingawa aliachiwa huru muda mfupi baadaye.
Habari zinadai kwamba Rubiales alikamatwa kwa tuhuma za kupokea rushwa wakati akiufanyia kazi mpango wa kuandaa mechi ya Spanish Super Cup mjini Riyadh, Saudi Arabia na waendesha mashtaka wanataka afungwe jela miaka miwili na nusu.
Rubiales ambaye amekana kufanya kosa lolote, alikamatwa mara baada ya ndege aliyosafiria kutua Madrid na kupelekwa moja kwa moja polisi kwa gari jeusi akiwa chini ya ulinzi wa maofisa kadhaa.
Chanzo kimoja cha habari Hispania kilieleza kuwa Rubiales anatarajia kufikishwa mahakamani Alhamisi hii huku pia ikidaiwa kwamba wakati akiwa Dominica, polisi waliivamia nyumba yake na kufanya upekuzi.
Ukiachana na sakata hilo jipya la rushwa, Rubiales anakabiliwa na kashfa ya udhalilishaji kijinsia kwa kitendo alichofanya Agosti mwaka jana cha kumbusu mdomoni hadharani mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania, Jenni Hermoso.
Rubiales akionekana mwenye furaha wakati wa hafla za kukabidhiwa tuzo za ushindi wa Kombe la Dunia la Wanawake mjini Sydney, Australia, alimkumbatia kwa nguvu na kumbusu mdomoni Jenni, tukio ambalo lilizua taharuki duniani kote.
Baada ya tukio hilo, Rubiales alijikuta akiandamwa kila kona na kushinikizwa kujiuzulu nafasi yake RFEF jambo ambalo awali alilikataa akidai kulikuwa na makubaliano baina yake na Jenni ingawa baadaye alitangaza kujiuzulu.