Na mwandishi wetu
Bao pekee la Fabrice Ngoma limeiwezesha Simba kutoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Tanzania na hivyo kujiimarisha katika mbio za kuliwania taji la Ligi Kuu NBC.
Katika mechi hiyo iliyochezwa leo Jumatatu, Mei 5, 2025 kwenye Uwanja wa Ismuhuyo, Dar es Salaam, bao hilo lilipatikana muda mfupi kabla ya timu kwenda mapumziko baada ya Ngoma kuinasa pasi ya Steven Mukwala.
Kwa ushindi huo Simba ambao pia wanajiandaa kwa mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco, sasa wamefikisha pointi 63 katika mechi 24 walizocheza.
Timu hiyo hata hivyo bado ina kazi ya kufanya kuwaondoa mahasimu wa Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 70 katika mechi 26.
Kimahesabu Simba watakuwa na kazi nzito ya kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizobaki ikiwamo mechi yao na Yanga ili kujihakikishia taji la ligi hiyo.
Kwa upande wa JKT wao wanabaki katika nafasi ya saba wakiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 27.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids baada ya mechi hiyo aliwapongeza wachezaji wake kwa namna walivyopambana na kufanya juhudi hadi kupata ushindi huku akisema kwamba mechi ilikuwa ngumu.
Naye kocha wa JKT, Ahmad Ally alisema kwamba makosa madogo waliyoyafanya dakika za mwisho mwisho za kipindi cha kwanza ndiyo yaliyowafanya waadhibiwe na Simba.
Soka Ngoma aizamisha JKT Tanzania
Ngoma aizamisha JKT Tanzania
Read also
