Manchester, England
Baada ya kuichapa Arsenal mabao 4-1, kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema kwamba upepo wa taji la Ligi Kuu England (EPL) hatimaye umehamia upande wao na wana nafasi ya kulibeba taji hilo.
Wiki kadhaa zilizopita, Pep amekuwa akiipa Arsenal nafasi kubwa ya kulibeba taji hilo lakini baada ya ushindi huo na kupunguza tofauti ya pointi hadi kubaki mbili, kocha huyo sasa amebadili kauli.
Badala yake Pep anaamini Man City ambayo pia imezidiwa mechi mbili na Arsenal ipo katika nafasi nzuri ya kulibeba taji msimu huu na hivyo kuweka rekodi ya kulibeba mara tano katika misimu sita.
Kwa sasa Arsenal ndiyo inayoshika usukani wa ligi hiyo lakini Pep anaamini kwamba taji la ubingwa wa ligi hiyo kwa sasa lipo kwenye himaya ya timu yake.
Pep hata hivyo alionekana kuwa makini na kauli hiyo aliposema suala la kulibeba taji litategemea na wao wenyewe kwani wanalazimika kushinda mechi zilizo mbele yao na kwa sasa anaitaka nafasi inayoshikiliwa na Arsenal.
“Mechi tatu zijazo ni muhimu mno, Jumapili na Fulham na baada ya hapo mechi mbili za nyumbani, hizi mechi tatu zitaamua nini tunachokifanya, inaonekana kituko lakini kwa sasa tupo nyuma ya Arsenal, wametuzidi kwa pointi mbili,” alisema Pep.
Man City ilipata ushindi huo ikineemeka kwa mabao mawili ya Kevin De Bruyne na mengine mawili ya John Stones na Erling Haaland wakati bao pekee la Arsenal lilifungwa na Rob Holding.
Kwa upande wake kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema licha ya timu yake kufungwa mabao mengi bado hajaitoa timu hiyo katika mbio za kulibeba taji la EPL badala yake alisema wanalazimika kushinda mechi zote tano zilizobaki ili waweze kumaliza ligi mbele ya City.
“Tunataka kupambana, hatutokata tamaa, ni kwenye mechi tano na lolote linaweza kutokea kwenye ligi hii, tumefungwa na timu bora, hilo halina ubishi,” alisema Arteta.