Davos, Uswisi
Rais wa Fifa, Gianni Infantino (pichani) amesema kwamba nchi ya Iran itacheza mechi zake za fainali za Kombe la Dunia nchini Marekani kama ilivyopangwa.
Kumekuwa na hofu juu ya ushiriki wa Iran kwenye faianli za Kombe la Dunia zitakazoanza kutimua vumbi Juni 11, 2026 katika nchi za Marekani, Canada na Mexico kutokana na vita inayoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Shirikisho la Soka Iran hivi karibuni lilitoa taarifa likidai kwamba linafanya mazungumzo na Fifa ili mechi zao zisichezewe nchini Marekani badala yake zihamishiwe Mexico.
Taarifa ya shirikisho hilo inahusishwa na kauli iliyowahi kutolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye alisema kwamba anaikaribisha Iran nchini Marekani lakini hawezi kuihakikishia usalama.
Kwa upande mwingine kauli ya Infantino kuthibitisha ushiriki wa Iran inatafsiriwa kuwa huenda imetokana na mazungumzo na Shirkisho la Soka Iran na hivyo ushiriki wa Iran kwenye fainali hizo utakuwa kama ilivyopangwa na Fifa.
“Iran itakuwapo kwenye Kombe la Dunia, tuna furaha kwa sababu wana timu imara sana, nina furaha kwa hilo, mechi zitachezwa pale zinapotakiwa kuchezwa kwa mujibu wa ratiba,” alisema Infantino.
Iran itaanza mechi zake kwa kuivaa New Zealand na baadaye Ubelgiji, mechi zitakazochezwa mjini Los Angeles Juni 15 na Juni 21 na Juni 26 itacheza na Misri mjini Seattle.
Naye Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum alisema kwamba nchi yake inajiandaa kuikaribisha Iran kucheza mechi zake za Kombe la Dunia katika taifa hilo.
Kauli ya Rais wa Mexico inapingana na ile ya Infantino ambaye alishuhudia Iran ikiichapa Costa Rica mabao 5-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa nchini Uturuki.
Baada ya mechi hiyo Infantino alisisitiza kwamba Iran itashiriki fainali za Kombe la Dunia kama ilivyopangwa na ameiona timu, amezungumza na wachezaji na kila kitu kipo sawa.
