Na mwandishi wetu
Katika mkakati wa kusaka matokeo mazuri, uongozi wa klabu ya Yanga umeamua kuliongezea nguvu benchi la ufundi na kumtangaza Abdihamid Moalin kuwa kocha msaidizi ambaye atamsaidia kocha mkuu, Pedro Cooncalves.
Moalin ambaye si jina geni katika soka la Tanzania amekabidhiwa jukumu hilo baada ya kuwapo minong’ono kuhusu kutimuliwa kwa Pedro kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika mechi za hivi karibuni.
Yanga licha ya kuwa inashika usukani katika Ligi Kuu NBC, hivi karibuni imeandamwa na matokeo ya sare jambo ambalo limewafanya baadhi ya mashabiki kuhoji mwelekeo wa timu yao huku wengine wakitaka Pedro atimuliwe.
Katika mechi hizo Yanga imetoka sare ya bila kufungana na Simba, baada ya hapo ikapata sare na Azam FC, Mtibwa Sugar na TRA United na kuvuna pointi nne katika mechi hizo nne badala ya 12 ambazo zilitarajiwa.
Uamuzi wa kumtangaza Moalin kuwa kocha msaidizi umetokana na kikao cha uongozi wa klabu hiyo kilichofanyika Jumatatu Machi 23, 2026 na taarifa yake kupatikana jioni ya siku hiyo hiyo.
Moalin ambaye amewahi kuinoa Azam, pia aliwahi kuwa kocha msaidizi na mkurugenzi wa ufundi wa Yanga kwa vipindi tofauti chini ya makocha Sead Ramovic na Miloud Hamdi.
Akiwa Yanga, Moalini alipata mafanikio msimu wa 2024-25 kwa kubeba mataji ya Ligi Kuu NBC, Kombe la Shirikisho CRDB na lile la Ligi ya Muungano.
Taarifa ya Yanga pia imebainisha namna timu inavyopitia kipindi kigumu ikiwa na wachezaji wengi majeruhi na hivyo kuwa sababu mojawapo ya kushindwa kupata matokeo mazuri na katika kukabiliana na hilo uongozi umeamua kuliimarisha benchi la ufundi.
Wachezaji ambao wanatajwa kuwa ni majeruhi ni pamoja na Prince Dube, Depu, Ibra Bacca, Khomein Aboubakar, Clement Mzize, Shadrack Boka, Dickson Job na Edmund John.
Changamoto nyingine iliyoelezwa katika taarifa hiyo ni timu kucheza mechi saba katika kipindi cha siku 21 huku ikilazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya mechi hizo jambo ambalo lilipunguza ufanisi kwa wachezaji.
Soka Moalin kumsaidia Pedro Yanga
Moalin kumsaidia Pedro Yanga
Read also
