Na mwandishi wetu
Simba haijakata tamaa katika mapambano ya kuishusha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC na hata kubeba taji hilo baada ya kuinyuka Pamba Jiji FC mabao 2-1.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Juni 14, 2026 kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam, Simba ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya nane lililofungwa na Elly Mpanzu akiitumia pasi ya Neo Maema.
Pamba hawakutetereka baada ya kufungwa bao hilo, walionesha utulivu na kutengeneza mashambulizi na juhudi zao kuzaa matunda katika dakika ya 18 kwa bao lililofungwa na Mathew Momanyi.
Tamaa ya Simba kutoka uwanjani na pointi tatu ilijidhihirisha kwa namna ambavyo walionesha umakini wakitawala eneo la kiungo na hatimaye kupata bao la ushindi katika dakika ya 65, bao lililofungwa na Libasse Gueye.
Kwa ushindi huo Simba inaendelea kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 61 ikiwa imezidiwa na mahasimu wao Yanga wanaoshika usukani wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi mbili hali inayoonesha kuwa nafasi ya kulibeba taji la ligi hiyo bado ipo wazi.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Tanzania Prisons ilifanikiwa kutoka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Matokeo hayo ni mwanzo mzuri kwa Prisons ambao wanahaha kujinasua na janga la kushuka daraja wakiwa nafasi ya 15 na pointi zao 23 baada ya kucheza mechi 26.
Kimataifa Simba yapambana kuitoa Yanga kileleni
Simba yapambana kuitoa Yanga kileleni
Related posts
Read also
