Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe amesea alijua kabla kuwa Lionel Messi angeshinda tuzo ya Ballon d’Or baada ya kuiwezesha Argentina kubeba Kombe la Dunia 2022.
Mbappe ambaye alifunga mabao matatu (hat trick) katika mechi ya fainali, mabao ambayo hata hivyo hayakuweza kuizuia Argentina kuipiku Ufaransa na kubeba taji la dunia kupitia mikwaju ya penalti.
“Nilijua atashinda siku ile ile usiku wa mechi ya fainali, Messi alikuwa na sifa hiyo, kama alishinda Kombe la Dunia alitakiwa pia kushinda Ballon d’Or. Ni mmoja wa wachezaji bora katika historia kama si ndiye bora,” alisema Mbappe.
Messi, ambaye pia alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa fainali hizo zilizofanyika Qatar akiwa amefunga mabao saba, kwa Ballon d’Or hiyo ni ya nane na aliishinda akiwabwaga Mbappe na mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland.
Wapo ambao walihoji kwa nini Messi alitwaa tuzo hiyo na si Haaland aliyemaliza msimu na mabao 51 na kuiwezesha Man City kubeba mataji ya Ligi Kuu England, FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya au Mbappe aliyekuwa na mabao 34 katika mechi 29 za ligi na kuiwezesha PSG kubeba taji la Ligi 1.
Akijibu hoja hiyo Mbappe anasema kwamba hapo hakuna cha kujadili licha ya ukweli kwamba yeye na Haaland walikuwa na msimu mzuri.
“Ni kweli kwamba mimi na Haaland tulikuwa na msimu mzuri lakini hiyo si zaidi ya Kombe la Dunia ambalo Messi alishinda, huwezi kulinganisha,” alifafanua Mbappe.
.