Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Simba imepigwa marufuku kufanya usajili wa wachezaji hadi itakapoilipa klabu ya Teungueth ya Senegal pesa za usajili wa mchezaji Pape Sakho iliyomsajili kutoka timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF iliyopatikana leo Alhamisi, uamuzi huo umefikiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) baada ya klabu ya Teungueth kushinda kesi ya madai ya mauzo ya mchezaji huyo.
Sakho ambaye kwa sasa anaichezea Quevilly Metropole ya Ufaransa, aliichezea Simba kabla ya kutimkia Ufaransa ambapo katika madai yao, Teungueth walitaka Simba iwalipe sehemu ya malipo baada ya kumuuza mchezaji huyo katika klabu ya Quevilly.
Simba ilipewa siku 45 kuhakikisha inafanya malipo hayo lakini haikufanya hivyo na hatimaye uamuzi mgumu umefikiwa na sasa watalazimika kukamilisha malipo hayo kama watahitaji kukiongezea nguvu kikosi chao ambacho kinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kikiwa katika hatua ya makundi.
Uamuzi wa Fifa kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TFF iliyosainiwa na ofisa habari na mawasiliano wa shirikisho hilo, Cliford Ndimbo, unahusu usajili wa wachezaji kimataifa lakini TFF wameiongezea nguvu adhabu hiyo kwa kuipiga marufuku Simba kufanya usajili wa ndani.
Sakho akiwa na Simba takriban misimu miwili iliyopita alitoa mchango mkubwa katika timu hiyo kwenye Ligi Kuu NBC, Ligi ya Mabingwa Afrika na michuano mingine akiwa mmoja wa wachezaji muhimu.
Mchezaji huyo pia aling’ara Afrika katika tuzo za wanamichezo bora Afrika kwa kubeba tuzo ya bao bora iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika katika hafla iliyofanyika mjini Rabat, Morocco.
Tuzo hiyo aliipata baada ya kufunga bao zuri la ‘tik-taka’ katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, mechi ambayo Simba ilitoka na ushindi wa mabao 3-1.
Kimataifa Sakho aiponza Simba, Fifa yaizuia kusajili
Sakho aiponza Simba, Fifa yaizuia kusajili
Read also