Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo akiwataka wasiwe na hofu kwa sasa hata baada ya kuondoka kwa kocha mkuu wa tim hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Robertinho ameondoka nchini juzi Jumatatu akielekea kwao Brazil kwa matatizo ya kifamilia na anatarajiwa kurejea mwishoni mwa mwezi huu kuendelea na majukumu yake.
Kuondoka kwa kocha huyo kumeibua taharuki na wasiwasi kwa mashabiki wa timu hiyo wakihisi pengine kocha huyo anaweza asirejee au akatumia muda mrefu wakati timu hiyo ikikabiliwa na mechi za mashindano makubwa hivi karibuni.
Mgunda amewahakikishia kuwa timu hiyo ipo katika mikono salama na yeye na wenzake wa benchi la ufundi watahakikisha wanaiandaa vizuri timu hiyo hadi kocha huyo atakaporudi.
“Najua hofu waliyokuwa nayo mashabiki lakini niwatoe hofu kwamba timu yao ipo katika mikono salama na hakuna kitakachoharibika, tutaiandaa vizuri timu kimashindano kulingana na michuano tuliyonayo mpaka kocha mkuu atakaporudi mwishoni mwa mwezi huu,” alisema Mgunda.
Kocha huyo ameeleza kuwa Robertinho, alipoondoka aliacha programu za mazoezi na pia amekuwa akipiga simu kila siku kuulizia maendeleo na uwajibikaji wa wachezaji hivyo haoni sababu ya mashabiki wao kuwa na presha wakati huu ambao kocha hayupo lakini wanashirikiana kwa kiasi kikubwa kuhakikisha hakuna kinachoyumba.
Mgunda alisema hiki ni kipindi muhimu kwao kujenga umoja na mshikamano na kuisapoti timu yao katika vita kali iliyopo mbele yao ya kupigania ubingwa wa Ligi Kuu NBC na kufika mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo mashabiki wanapaswa kuwa na imani na timu yao na kuwasapoti makocha waliopo.
Simba iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC, ikizidiwa pointi sita na vinara Yanga, inajipanga kwa ajili ya mechi za Kombe la FA za raundi ya tatu ambapo wataumana na Coastal Union na mechi za Ligi ya Mabingwa za hatua ya makundi zitakazoanza kuunguruma Februari, mwaka huu
