Na mwandishi wetu
Wakati Ligi Kuu NBC ikielekea kwenye mechi za raundi ya 20, Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Pluijm ameeleza wazi kuipa Yanga nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wake msimu huu.
Kwa sasa Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa imekusanya pointi 50, baada ya mechi 19 ambazo wamecheza mpaka sasa, wakifuatiwa na Simba iliyokusanya pointi 44 katika nafasi ya pili.
Pluijm ameiambia GreenSports sababu za kuipa Yanga nafasi ya ubingwa ni kutokana na upambanaji na ubora wa kikosi ilichonacho hivi sasa ukilinganisha na timu nyingine 15 zinazoshiriki ligi hiyo.
“Niwe mkweli Yanga ndio timu yenye wachezaji wenye viwango vya juu kwenye ligi ya Tanzania msimu huu na kwa hilo wanastaili kutetea ubingwa wao kutokana na matokeo wanayoendelea kuyapata katika mechi zao,” alisema Pluijm.
Kocha huyo wa zamani wa Azam alisema kiashiria cha kuonesha kwamba timu hiyo ni bora na inastahili kuwa bingwa msimu huu ni mwenendo wake tangu kuanza kwa msimu huu lakini pia ndio timu pekee iliyodondosha pointi chache ukilinganisha na timu nyingine zilizosalia.
Pluijm raia wa Uholanzi alisema hata wapinzani wa Yanga, Simba hawana uwezo wa kuipiku Yanga kwenye mbio za ubingwa msimu huu hata matokeo wanayoyapata kwenye ligi ni kama wanawasindikiza katika mbio hizo za taji lao la pili mfululizo.
“Kwa maoni yangu, nafikiri Simba hawatashinda kwenye mbio hizi msimu huu pia kutokana na mwenendo ulivyo wa ligi, lakini nasi tumekuwa na mipango yetu ya kupigania kumaliza kwenye nafasi ya tatu au ya nne, tunapambana tusitoke hapo,” alisema Pluijm.
