Milan, Italia
Mshambuliaji wa Inter Milan, Romelu Lukaku ametaka mabosi wa Serie A wachukue hatua baada ya kufanyiwa vitendo vya dhihaka za ubaguzi wa rangi na mashabiki wa Juventus juzi Jumanne.
Lukaku anayeichezea Inter kwa mkopo akitokea Chelsea alipewa kadi ya pili ya njano kwa kosa la kuwatolea mashabiki ishara ya kuwataka wakae kimya baada ya kufunga bao katika dakika tano za nyongeza.
Lukaku alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti katika mechi ya Coppa Italia na katika hali ya furaha ndipo alipowaonyesha mashabiki ishara hiyo ya kuwataka wakae kimya na mwamuzi akampa kadi.
“Historia inajirudia, nimekuwa katika matukio haya mwaka 2019 na kwa mara nyingine tena mwaka 2023, huu mchezo mzuri lazima ufurahiwe na kila mtu, natumaini wasimamizi wa ligi safari hii watachukua hatua stahiki.” alisema Lukaku.
Uongozi wa klabu ya Juventus umeahidi kutoa ushirikiano kwa polisi ili kuwabaini mashabiki waliohusika katika tukio hilo ambalo pia liliandamana na mzozo baina ya wachezaji wa timu zote mbili mara baada ya bao hilo la kusawazisha lililofungwa na Lukaku.
Katika mzozo wa wachezaji, nahodha wa Inter, Samir Handanovic na kiungo Juan Cuadrado walipewa kadi nyekundu kila mmoja baada ya kuibuka mzozo wakati wachezaji wakielekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Lukaku ambaye alijiunga na Inter majira ya kiangazi msimu uliopita, aliwahi kukutana na kadhia hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2019 na baadaye mwaka 2021.
Aliwahi kuzungumzia matukio ya aina hiyo Septemba 2019 akidai kwamba mchezo wa soka unarudi nyuma kutokana na matukio ya aina hiyo.