Na mwandishi wetu
Mechi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu baina ya mahasimu Yanga na Simba
imemalizika jana pale Uwanja wa Mkapa, Temeke, Dar es Salaam kwa
suluhu.
Mbali na ukongwe, wingi wa mashabiki, ubora wa vikosi kwa sasa ilikuwa
chachu nyingine ya mashabiki na wapenda soka Afrika Mashariki na Kati
kuitamani mechi hiyo.
Yanga msimu huu si ile ya misimu kadhaa nyuma, ipo vizuri, inaongoza
msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Bara kwa pointi 55 dhidi ya Simba yenye 42,
anayefuatia ni Namungo ana pointi 29.
Simba haihitaji sana maelezo kwa wanachokifanya kwa takriban msimu wa
tano sasa. Wameitetemesha ligi kwa misimu minne mfululizo kabla ya
Yanga kuingilia kati ubabe huo msimu huu lakini pia imetoka kupambana
kabla ya kutolewa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa
matuta 4-3 na Orlando Pirates baada ya ushindi wa bao 1-0 la nyumbani
kwa kila timu.

Waliheshimiana kupita kiasi
Unaweza pia kusema walikuwa wakiviziana. Mashabiki wengi waliokwenda
uwanjani na waliobaki kuangalia kwenye runinga walitegemea kuona kitu
tofauti baada ya mechi ya kwanza kuisha kwa suluhu lakini imekuwa
tofauti.
Kwa vikosi vyote viwili kuwa na heshima ya woga wa kuvizia kutoruhusu
makosa hata ya kawaida kimpira yalipelekea mechi hiyo kuwa ya kawaida,
kuondoa hisia zilizokuwa zinafikirika na mwisho kuwafanya wadau,
mashabiki na pengine hata viongozi wa timu hizo kutoamini macho yao
kwamba ile mechi moja inayosubiriwa kwa msimu mzima wameishuhudia
ikiwa ya kawaida kabisa.
Kusubiri kwa dakika 73 kabla ya kupigwa shambulio la kwanza
lililolenga goli kwa timu zote mbili ilitosha kuonesha jinsi gani
ilikuwa ni mechi iliyokosa ‘amsha amsha’.
Chris Mugalu wa Simba ndiye aliyekuwa wa kwanza dakika ya 74 kupiga
kichwa ndani ya boksi la Yanga kilichodunda na kutua mikononi mwa kipa
wa Yanga, Djigui Diarra. Mpira huo ulipigwa krosi ikiwa ni faulo
iliyochongwa na Shomari Kapombe. Hata shambulio lenyewe si umeona
mazingira yake. Msisimko wa derby haukuwa kwenye ubora wake stahiki.
Mbwembwe eneo la kati
Mpira ukishakuwa hauna mashambulizi ya kila wakati na hasa kutolenga
lango maana yake mpira unachezwa zaidi pembeni na katikati ya uwanja
na ndiko angalau ilipatikana burudani ya soka.
Chenga ya Clatous Chama iliyomfanya Feisal Salum ‘Fei Toto’ akateleza
na kugaagaa akiufuata mpira kwa taabu au Fei alipomvisha kanzu Shamori
Kapombe na ‘kuu-control’ mpira kwa madaha kabla ya kutoa pasi. Angalau
kwa upande huo kulikuwa na ladha.
Kesi ya Mayele, Inonga
Kesi ya mshambuliaji tishio, Fiston Mayele dhidi ya Henock Inonga
iliendelea kama kawaida baada ya ile ya mechi ya awali ambayo Inonga
aliibuka shujaa ‘akitembea’ na mshambuliaji huyo kila kona ilimradi
asifunge na dakika ya 83 alimsindikiza mpaka mwisho wakati akifanyiwa
mabadiliko ya kuingia Herritier Makambo.
Kwa mara nyingine katika mechi ya jana, Inonga aliibuka mbabe mbele ya
Mayele ambaye alipiga shuti moja tu kipindi cha pili lililogonga nyavu
za nje ya lango. Mara zote walipokuwa wakikutana kwenye vita ya mmoja
mmoja, Inonga alishinda vita hiyo na hata alipokuwa akifanya
‘takolini’ zenye maamuzi magumu bado alicheza kwa ufasaha dhidi ya
mpinzani wake huyo.
Kwa kifupi ulikuwa ni mwendelezo wa vita yao waliyoianza DR Congo
wakati Mayele anakipiga AS Vita na Inonga yupo DC Motema Pembe na sasa
ipo ndani ya Derby ya Kariakoo kwa misimu kadhaa mbele. Bado kuna muda
wa kuendelea kuishuhudia burudani ya wawili hawa pale kwa Mkapa.
Kibwana Shomari kadhihirisha ubora
Beki wa kulia wa Yanga anayetumika kama beki wa kushoto kwa sasa,
Kibwana Shomari alionesha ubora wake vilivyo na kuonesha kwa nini
ameendelea kudumu kwenye kikosi hicho katika namba tofauti na
anayofahamika kucheza.
Mapema msimu huu, Yanga ilipomsajili beki wa kulia Shaban Djuma
ilionekana kama Kibwana anakwenda kusahaulika lakini badala yake akawa
anapangwa nafasi ya kushoto na akawa anacheza kwenye ubora mkubwa na
mwisho jana amedhihirisha hilo kwenye mechi kubwa dhidi ya wachezaji
wakubwa.
Alicheza nafasi yake kwa ubora na kumdhibiti Bernard Morrison asilete
madhara kabla ya kwenda nje na alipokuja Kibu Denis kazi ikawa ile
ile. Shomari akaendelea kuwa mwamba mpaka mwisho kwa kufanya majukumu
yake bila presha. Aliumudu mchezo kuliko ilivyotegemewa na wengi.
Simba yashindwa kutibua rekodi
Matokeo ya jana imeifanya Yanga iongeze sare nyingine na kufikia nne,
ushindi mechi 17 ikiwa haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa huku
wakibakiza mechi tisa kabla ya kufunga pazia la ligi.
Baada ya timu nyingine kushindwa kuifanya kazi ya kuifunga Yanga na
kuonekana hakuna anayeweza kuondoka na pointi tatu mbele yake msimu
huu, Simba ilibaki kuwa tegemeo kubwa la kutibua rekodi hiyo lakini
nao dakika zao 90 zimekwisha.
Ubingwa wacheleweshwa
Pamoja na yote, matokeo ya jana pia yamefanya ubingwa wa mapema kwa
Yanga msimu huu uchelewe kidogo kwani pengo la pointi ambalo Yanga
walikuwa na matumaini ya kuliweka kama wangeibuka na ushindi
limeshindwa kukamilika.
Tofauti ya pointi zimebaki zile zile 13 na kulingana na idadi ya mechi
10 ambazo wamebakiza Simba, bado ni mapema kidogo kuzungumzia ubingwa
kwa Yanga ingawa dalili zote zinaonesha ni suala la muda tu kabla ya
kutawazwa kuwa mabingwa mara 28 wa michuano hiyo.
Zogo kuhamia nusu fainali
Baada ya kukosekana mbabe wa mechi mbili za ligi, sasa imesalia mechi
moja ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam.
Yanga imetangulia nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuifunga Geita
Gold kwa mikwaju ta penalti 7-6 baada ya matokeo ya sare ya 1-1 ya
dakika 90 za awali na inasubiri mshindi wa mechi ya robo fainali baina
ya Simba na Pamba.
Simba imeeleza kuhitaji ushindi wa mechi hiyo na Yanga imekuwa
ikijinasibu kumsubiri Mnyama apenye ili wakutane amwoneshe, hivyo nalo
ni suala la kusubiri kama itakuwa hivyo.
Kama mechi hii itatimia ni wazi itatoa mshindi wa msimu baina yao
kwani si ya kugawana pointi bali itahitaji mshindi aidha katika dakika
90 au kwa njia ya penalti ili apatikane atakayekwenda kukipiga fainali
za michuano hiyo dhidi ya mshindi wa nusu fainali ya Coastal Union na
Azam FC.
