Doha, Qatar
Brazil yenye Neymar, moja ya timu inayopewa nafasi kubwa kubeba taji la Dunia, leo Ijumaa jioni katika mechi ya robo fainali inaumana na Croatia ya Luka Modric ambayo imejijengea sifa ya kujiamini na kufanya maajabu.
Ni mpambano wa timu mbili zenye uwezo na zilizokamilika kila idara, moja yaani Brazil historia yake imeendelea kuwa kubwa ikiwa na mataji matano ya dunia, imesheheni mastaa na ndio maana inapewa nafasi kubwa kubeba taji lakini nyingine inajulikana kwa kufanya maajabu.
Unapoyazungumzia maajabu ya Croatia katika michuano mikubwa, mmoja wa watu muhimu na kinara wa maajabu hayo ni Modric, mkongwe mwenye miaka 37 ambaye ameendelea kudhihirisha umahiri wake katika kulitawala dimba la kati.
Modric ambaye pia anaichezea Real Madrid ya Hispana ndiye aliyeiongoza vyema Croatia kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 kwa kufanya maajabu hadi kufikia hatua ya fainali katika hali ambayo haikutarajiwa na walio wengi.
Kama ambavyo Brazil inapewa nafasi ya kulibeba taji, wanaoijua vyema Croatia wanaichukulia kauli hiyo kwa tahadhari kwa kuwa mtihani wa leo wa Brazil ni mgumu, inakutana na timu ambayo pia ina uwezo kisoka lakini inasifika kwa kufanya maajabu.
Shauku kubwa ya Croatia kwa sasa ni kufanya maajabu zaidi ya yale waliyoyafanya 2018 kwa kufika fainali bila kutarajiwa na wengi, na sasa wanachotaka ni kombe na kama watauvuka mtihani wa leo hapana shaka kila mtu ataamini wana uwezo wa kubeba kombe na kuondoka Qaatar wakiwa mashujaa wapya wa dunia.
Kwa Modric hilo litakuwa na maana kubwa kwani huenda hizi zikawa fainali zake za mwisho za Kombe la Dunia au ni michuano mikubwa ya mwisho akiwa na jezi ya Croatia hivyo mafanikio yatakuwa na maana kubwa kwake, anaweza kucheza Euro 2024 kwani anaonekana kuwa na nguvu lakini Kombe la Dunia 2026 kidogo kuna ugumu.

Kimsingi hana atakachopoteza hizi zikiwa fainali zake za mwisho za Kombe la Dunia au michuano yake ya mwisho na timu ya Croatia, amecheza mechi 159 hadi sasa na timu ya Croatia, ni mechi nyingi na akiifikisha Croatia fainali atakuwa amefikisha mechi 162, lakini yote hayo yanaweza kufanikiwa iwapo ataanza kwa kushinda mtihani wa leo.
Sifa ambazo Modric amekuwa akipewa za kuwa kichwa katika kuipanga na kuilisha safu ya ushambuliaji ya Croatia kama kuna siku sifa hizo zinatakiwa kudhihirishwa na kuwa jambo kubwa zaidi basi siku hiyo inaanzia leo katika mtihani dhidi ya Brazil au Samba Boys.
Ukimuacha Modric, kipa wa Croatia ambaye pia anaichezea klabu ya Dinamo Zagreb, Dominik Livakovic naye ni mchezaji muhimu wa timu hiyo, tayari ameonyesha maajabu yake mbele ya Japan kwa kuokoa penalti tatu ambazo zimeipa timu hiyo tiketi ya robo fainali na hatimaye leo imeangukia mikononi mwa Brazil.
Neymar naye ni mtu mwingine ambaye mechi ya leo ina maana kubwa kwake, amewahi kusema kuwa hana uhakika kama ataendelea kuwa na timu ya Brazil hapo baadaye, huenda hizi ni fainali za mwisho kwake, hivyo wanaosubiri maajabu ya Croatia watambue Brazil ina Neymar ambaye atapenda kumaliza kishujaa lakini ushujaa huo unatakiwa kuanza kuonekana leo mbele ya Croatia.
