Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameuomba uongozi kumtafutia mechi moja ya kimataifa ya kirafiki kabla ya kukutana na CR Belouizdad katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga ipo kambini kwa sasa ikiendelea kujifua kujiandaa na mchezo huo wa kwanza ambao utachezwa Algeria, Novemba 24, mwaka huu na miamba hiyo imekusudia kushinda mchezo huo.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema kitendo cha kukaa wiki mbili bila mechi yoyote ya ushindani kinaweza kuathiri kasi yao ya uchezaji ndio maana anataka mechi moja ya ushindani ili kukiweka tayari kikosi chake.
“Tuna wiki mbili ambazo tutakaa bila kucheza mechi yoyote ya mashindano zaidi ya kufanya mazoezi, ndio maana nimeuomba uongozi kututafutia mechi moja ya kirafiki ya kimataifa ambayo itatuweka sawa kabla ya kucheza na Belouizdad Novemba 24,” alisema Gamondi.
Kocha huyo aliyewahi kuinoa Belouizdad alisema wapinzani wake hao ni timu ngumu na wana wachezaji wazuri lakini watajitahidi kutumia mbinu zake kuwakabili na kupata ushindi wakiwa ugenini.
Alisema tayari wameanza kuwafuatilia ikiwemo kumtuma mtaalamu wa kuchambua video (Video Analyst) ili kujua mbinu na vitu muhimu vya ndani ya uwanja wanavyotumia Belouizdad.
