Na mwandishi wetu
Mtibwa Sugar ambayo imenusurika kushuka daraja, imeanza harakati za kujiimarisha kwa msimu wa 2022/23 kwa kutangaza kumsajili beki wa kati, Iddy Mobby aliyekuwa akikipiga Ruvu Shooting.
Mtibwa ililazimika kucheza mechi mbili za mtoano dhidi ya Tanzania Prisons, imetamba kuwa usajili wa Mobby ni mwanzo tu na kwamba wanatarajia kuanika vifaa vyao vingine hivi karibuni.
Imeelezwa kuwa Mobby aliyewahi kuzitumikia pia Stand United, Mwadui na Polisi Tanzania ametua Mtibwa yenye maskani yake Manungu, Turiani mkoani Morogoro kwa mkataba wa miaka miwili.
“Usajili wake umeangalia zaidi pia mchango wake kwenye Ligi Kuu, ni mchezaji mzoefu na ligi ya sasa inataka watu wa hivyo, kocha Mayanga (Salum) anaendelea kuunda kikosi chake kikamilifu hatuhitaji kucheza ‘play-off’ kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita,” alisema Ofisa Habari wa Mtibwa, Thobias Kifaru.
“Ligi ya sasa haihitaji kuleta vijana wengi kuwavumilia. Tumeachana na wachezaji wengi hivyo ni lazima tuimarishe kikosi chetu kwa umakini mkubwa na sasa ndiyo tumeanza tutaendelea kuonesha zaidi vyuma vyetu vipya hivi karibuni,” alihitimisha Kifaru.
Mbali na mchezaji huyo pia inafahamika kwamba Mtibwa imeshamalizana na kipa wa zamani wa Yanga na KMC, Faroukh Shikalo na muda wowote atatua nchini kuungana na timu hiyo, pia imemalizana na kiungo wa zamani wa Yanga, Baraka Mapinduzi na mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Adam Adam.
Soka Mobby atimkia Mtibwa Sugar
Mobby atimkia Mtibwa Sugar
Related posts
Read also