Na mwandishi wetu
Hatimaye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeiondolea kifungo cha kutosajili klabu ya Yanga baada ya kuelezwa kuwa imemaliza kumlipa aliyewahi kuwa mchezaji wake Gael Bigirimana raia wa Burundi.
Yanga imefunguliwa ikiwa ni takriban miezi minne imepita tangu ilipofungiwa na Fifa kufanya usajili wa kimataifa huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiifungua kufanya usajili wa wachezaji wa ndani.
Kupitia taarifa rasmi ya TFF iliyowekwa leo Jumatano katika kurasa za mitandao ya kijamii ya shirikisho hilo, imefafanua kuwa Yanga imemalizana na mchezaji huyo aliyefungua kesi hiyo Fifa baada ya kuvunjiwa mkataba na waajiri wake hao.
“Awali mchezaji huyo (Bigirimana) alifungua kesi Fifa dhidi ya Yanga kwa kushindwa kumlipa baada ya kumvunjia mkataba.
“Bigirimana alishinda kesi hiyo, na Yanga ilitakiwa kumlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo wa Fifa ulipotolewa lakini haikutekeleza na kusababisha ifungiwe,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa maana hiyo, Yanga sasa inaweza kuendelea na harakati za kunasa nyota wanaotajwa kuwawania kwa ukaribu akiwemo mshambuliaji kutoka Ghana, Jonathan Sowah katika dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu na kufungwa Januari 16, mwakani.
Kimataifa Fifa yairuhusu Yanga kusajili
Fifa yairuhusu Yanga kusajili
Read also