Cairo, Misri
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Veron Mosengo-Omba (pichani) amejiuzulu nafasi hiyo wakati shirikisho hilo likiwa katika mgogoro baada ya Senegal kuvuliwa taji la ubingwa wa Afrika (Afcon 2025).
Senegal ambayo iliibuka kinara na kutangazwa mshindi wa taji hilo baada ya kupata ushindi katika mechi ya fainali dhidi ya wenyeji Morocco imevuliwa ushindi huo na kupewa Morocco sababu ikitajwa kuwa ni kitendo cha timu hiyo kugomea mechi hiyo kwa takriban dakika 17.
Mosengo-Omba, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambaye ameshika wadhifa huo kwa takriban miaka mitano, hata hivyo katika taarifa yake ya kujiuzulu hakutaja suala la Senegal.
Badala yake alisema kwa ufupi tu kuwa ameamua kujiuzulu ili awe na muda wa kutosha kwa ajili ya masuala yake binafsi.
“Kwa hili nimeweza kuvunja uvumi ambao baadhi ya watu wamekuwa nao kwa kiwango kikubwa wakinihusisha mimi, sasa nastaafu kwa amani ya moyo bila matatizo,” alisema Mosengo-Omba.
Naye Rais wa CAF, Dk Patrice Motsepe aliwaambia waandishi wa habari kuwa Mosengo-Omba amejiuzulu kwa lengo la kwenda kusaidia maendeleo ya soka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kuombwa na rais wa nchi hiyo, Felix Tshisekedi.
Dk Motsepe alimshukuru Mosengo-Omba kwa mchango wake na kazi aliyoifanya katika maendeleo na mafanikio ya soka la Afrika.
Kwa sasa nafasi ya Mosengo-Omba itashikwa kwa muda na mkurugenzi wa mashindano wa shirikisho hilo, Samson Adamu kutoka Nigeria ambapo Dk Motsepe amesema anaamini Adamu atafanya kazi nzuri na atasaidia kuifanya CAF ipige hatua mbele.
Dk Motsepe pia alisema kwamba makamu wa rais wa CAF wataongoza mchakato wa kumchagua katibu mkuu mpya na baada ya hapo ripoti ya mchakato huo itawasilishwa kwake (Dk Motseppe).
