Lausanne, Uswisi
Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) imesema inahitaji kupata bodi mpya sahihi ya kimataifa ya kusimamia mchezo wa ngumi vinginevyo iufute mchezo huo katika Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles, Marekani mwaka 2028.
IOC ilitangaza kulivua Shirikisho la Kimataifa la Ngumi (IBA) haki ya kusimamia ngumi katika Michezo ya Olimpili ya Tokyo mwaka 2021 na ile ya Paris ambayo inatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Juzi Jumanne Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhisho wa Michezo (CAS) ilitangaza kuunga mkono maamuzi ya IOC ya kutoitambua IBA na hata kuitoa moja kwa moja katika Olimpiki.
Kwa kipindi kirefu IOC imeelezea wasiwasi wake kuhusu uongozi wa IBA na nidhamu ya usimamizi katika mapambano ya ngumi namna mapambano hayo yanavyosimamiwa na majaji wake.
Mwaka jana viongozi wa IOC walimlalamikia Rais wa IBA-Urusi, Umar Kremlev kwa kutumia lugha za shari na vitisho kwa maofisa waandamizi wa IOC.
IOC imewataka viongozi wa mashirikisho ya ngumi kwa kila nchi na kamati za olimpiki kila nchi kusaidia kuundwa bodi mpya ya kimataifa ya kusimamia mchezo wa ngumi kwa lengo la kuupa nafasi mchezo huo katika Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles.
Katika agizo hilo IOC imetaka kuona inakuwa na mshirika wa ngumi kwenye Olimpiki ambaye ni bodi mpya ya kimataifa ya mchezo huo mapema mwaka 2025 ili kuupa nafasi mchezo huo kwenye Olimpiki.
IOC haijataja jina la bodi mpya lakini inadhaniwa huenda ikawa ni World Boxing, umoja ambao unaundwa na maofisa wa Marekani na Uingereza ambao mwaka jana walijitoa IBA na kumteua, Boris van der Vorst wa Uholanzi kuwa rais wao.
Ngumi Ngumi kufutwa kwenye Olimpiki?
Ngumi kufutwa kwenye Olimpiki?
Read also
