Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema sare ya mabao 2-2 waliyoipata jana Jumanne dhidi ya Namungo imewagusa na kuwaumiza mno hasa kwa namna walivyopoteza pointi tatu dakika chache kabla ya kumalizika kwa mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC.
Namungo walifuta ndoto za Simba kutoka na ushindi baada ya bao la kujifunga la Kennedy Juma dakika ya 90 katika harakati za kuokoa mpira uliochonganishwa langoni mwa Simba katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi.
“Niseme ndivyo mpira ulivyo, haiishi mpaka dakika 90 zikamilike maana ilibaki kama dakika mbili tu lakini goli linafungwa muda wowote, ni kweli inagusa, inauma na matokeo ya mpira ni katili lakini tumekubaliana nayo, tumejifunza, tunakwenda kukaa chini, kutafakari kujirekebisha ili kurejea kwenye matokeo mazuri na bora zaidi kwa timu,” alisema Mgunda.
Alisema pamoja na yote lakini walifahamu mchezo huo usingekuwa mwepesi kutokana na hali ilivyo kwenye msimamo wa ligi hasa ikizingatiwa kuwa ligi inaelekea ukiongoni kwa sasa na wao wanachukua matokeo hayo kama funzo.
Mgunda alisisitiza kuwa wanakwenda kujipanga zaidi kwenye uwanja wa mazoezi ili kutafuta matokeo yenye afya kwa timu hiyo katika mechi zilizosalia kabla ya kufungwa rasmi kwa pazia la ligi.
Naye kocha mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera alisema: “Sisi hatukuingia na pointi kwamba Simba imekuwa dhaifu au inashindwa kupambania ubingwa au vinginevyo. Tulijua dhidi ya Simba ni mechi ngumu sababu wametoka kuchukua Kombe la Muungano na walikuwa wanajiamini baada ya kuifunga Azam na kubeba lile kombe.
“Na kwenye ligi sababu Simba anapambania kupanda juu tukajua hawezi kuruhusu tena kupoteza pointi kwa hiyo hii mechi itakuwa ngumu, tukaiandaa timu kisaikolojia na kuwaambia wachezaji kwamba tupambane, tushikilie mbinu yetu.
“Na waiheshimu Simba kwa asilimia 80 na wakijitoa kweli, basi Mungu mwenyewe ataamua na hata tukifungwa tutajua tulifanya kile tulitaka, tukidroo tutajua kwamba tulijitolea tukafikia hapa, kwa hiyo kwangu nawapongeza wachezaji wangu, walijitoa sana.”
Kwa matokeo hayo, Simba imeendelea kusalia nafasi ya tatu kwa pointi zao 47 baada ya mechi 22 na Namumgo ambao katika mechi ya kwanza msimu huu walitoka sare ya bao 1-1 na Simba wameendelea kuganda nafasi ya tisa kwa pointi 27 baada ya mechi 24.
Soka Mgunda: Sare ya Namungo inauma
Mgunda: Sare ya Namungo inauma
Read also