Miami, Marekani
Mshambuliaji wa klabu ya Inter Miami ya Marekani, Luis Suarez amefungiwa mechi sita kwa kosa la kumtemea mate mmoja wa viongozi katika benchi la ufundi la klabu ya Seattle Sounders.
Tukio hilo lilitokea baada ya mechi ya Kombe la Ligi baina ya timu hizo iliyoisha kwa Sounders kutoka na ushindi wa mabao 3-0 ingawa baadaye Suarez alijilaumu kwa kosa hilo na kuomba msamaha.
Mara baada ya mwamuzi kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo, wachezaji na baadhi ya viongozi wa timu hizo mbili walianza kuzozana na kushikana na ndipo Suarez alipomtemea mate mmoja wa makocha wa timu pinzani.
Kabla ya tukio hilo, Suarez ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 38, alionekana akimkwida shingoni kiungo wa Sounders, Obed Vargas lakini wachezaji wanzake waliingilia kati.
Baada ya tukio hilo, Suarez alionekana kwa mara nyingine akizozana na mkurugenzi wa usalama wa Sounders, Gene Ramirez lakini mchezaji mwenzake Oscar Ustari alimzuia na ndipo mchezaji huyo alipoamua kumtemea mate mmoja wa makocha wa Sounders.
Kamati ya Nidhamu ya Kombe la Ligi katika taarifa yake ilifafanua kuwa adhabu ya Suarez itaanza kutumika mwakani katika michuano ya kombe hilo ingawa mamlaka za Ligi Kuu Marekani au Major League Soccer (MLS) nao wanaweza kumuongezea adhabu.
Sambamba na Suarez wachezaji wengine wa Inter Miami waliokumbana na adhabu ni Sergio Busquets aliyefungiwa mechi mbili na Tomas Aviles amefungiwa mechi tatu wakati mjumbe wa benchi la ufundi la Sounders, Steven Lenhart amefungiwa mechi tano.
Suarez, nyota wa zamani wa Liverpool na Barcelona amekuwa akiandamwa na matukio yaliyojaa utata, akiwa Liverpool alifungiwa mechi nane kwa kumfanyia dhihaka za ubaguzi wa rangi beki wa Man United Patrice Evra.
Mchezaji huyo pia amewahi kufungiwa kwa matukio matatu ya kuwang’ata wachezaji wa timu pinzani katika mechi wakati akizichezea timu za Ajax, Liverpool na timu yake ya taifa ya Uruguay.
Kimataifa Suarez afungiwa mechi sita
Suarez afungiwa mechi sita
Read also
