Miami, Marekani
Mshambuliaji wa timu ya Inter Miami ya Marekani, Luis Suarez (pichani) ameomba radhi kwa kitendo chake cha kumtemea mate mmoja wa watu wa benchi la ufundi la timu ya Seattle Sounders.
Suarez, mshambuliaji wa zamani wa timu za Barcelona na Liverpool, alifanya kitendo hicho atika mechi ya fainali ya ligi baina ya timu hizo, mechi ambayo Miami ililala kwa mabao 3-0.
Akizungumzia tukio lilivyokuwa Suarez alisema kulikuwa na mazingira ya kuvurugwa na kuchanganyikiwa baada ya mechi na kwamba tukio walilofanyiwa halikutakiwa kufanywa.
Suarez hata hivyo alisema kwamba mazingira ya tukio hilo bado hayatoshi kuwa sababu ya kitendo alichokifanya kwani hakikuwa sahihi na anaomba radhi kwa hilo.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ambapo uliibuka mzozo baina ya wachezaji wa timu hizo mbili hali iliyomtia hasira Suarez na ndipo alipofanya kosa hilo.
Katika mzozo wa wachezaji hao, Suarez alimkwida shingoni kiungo wa Sounders, Obed Vargas wakati huo huo mchezaji mwenzake Sergio Busquets naye aliingilia kati.
Muda mfupi baadaye, Suarez alianza kuzozana na makocha wa Sounders kabla ya kuzuiwa na mchezaji mwenzake, Oscar Ustari na ndipo mchezaji huyo alipomtemea mate mmoja wa makocha wa Sounders.
“Najisikia vibaya kwa kilichotokea, na sitaki kujinyima nafasi ya kukiri hilo na kuomba msamaha kwa kila mtu ambaye aliumizwa na kile nilichokifanya,” alisema Suarez.
Baada ya Suarez kuomba msamaha mjadala ulioibuka ni kuhusu adhabu atakayopewa mchezaji huyo ambaye pia aliwahi kuingia katika matatizo akihusishwa na matukio matatu ya kuwang’ata wachezaji wa timu pinzani wakati akiichezea Ajax, Liverpoo na timu yake ya taifa ya Uruguay.
Kimataifa Suarez amtemea mate kocha, aomba radhi
Suarez amtemea mate kocha, aomba radhi
Read also
