Roma, Italia
Kocha wa zamani wa Man United, Jose Mourinho amesema timu hiyo haiwezi kupata mafanikio kwa kuwa na wachezaji na maofisa ambao wameendelea kuwa hapo tangu wakati yeye akiwa kocha.
Mourinho alikuwa kocha Man United kati ya mwaka 2016 na 2018 na kuiwezesha kubeba mataji ya Europa Ligi na Carabao na kumaliza msimu wa 2017-18 katika nafasi ya pili nyuma ya Man City, kwa sasa anainoa AS Roma ya Italia.
“Bado wapo watu katika klabu ile na ninaposema watu namaanisha baadhi ya wachezaji na pia baadhi ya watu ambao si wachezaji ambao bado wapo wakati nikiwaambia Man United kwamba kuwa na watu hawa huwezi kamwe kufanya lolote, na bado wapo,” alisema Mourinho.
Mourinho pia alisema kwamba namna wachezaji wa Man United wanavyochukulia baada ya kufanyiwa mabadiliko ilimfanya atambue kuwa anatakiwa kubadilika katika mfumo wake wa kuongoza timu na kuendana na mazingira.
“Pale Man United, nambadili mchezaji wakati wa mapumziko, wakala wake anakuja na kunilaumu kwa unyanyasaji,” alisema Mourinho ambaye ana rekodi ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na klabu za FC Porto na Inter Milan.
“Nililazimika kubadilika, nazikumbuka nyakati hizo na huwa nacheka kuhusu nyakati hizo lakini ni nyakati tofauti,” alisema Mourinho.
Timu ya Mourinho ya sasa, AS Roma inashika nafasi ya saba katika Ligi Kuu Italia au Serie baada ya jana Jumapili kuchezea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Bologna.
Mourinho aliwahi kusema kwamba alikataa ofa ya kufanya kazi Saudi Arabia lakini baadaye alisema anashawishika kuamini kwamba kuna siku atafanya kazi katika nchi hiyo.