Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama amewashukuru wote waliomuwezesha kuondoka na tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Desemba wa Ligi Kuu NBC pamoja na tuzo ya mchezaji bora wa Simba kwa mwezi huo huku akiahidi kuendelea kufanya hivyo.
Chama alikabidhiwa tuzo yake hiyo ya Ligi Kuu juzi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam walipoumana na Mbeya City na Wekundu hao kutoka na ushinda wa mabao 3-2.
Kiungo huyo fundi kutoka Zambia ambaye pia ameshinda tuzo ya mashabiki wa Simba kwa mara ya pili mfululizo msimu huu baada ya kufanya hivyo Agosti mwaka jana, amesema anatambua lengo lake ni kuchukua kwa mara nyingine zaidi tuzo hiyo kwani hayo ni miongoni mwa matunda ya kazi yake.
“Kwanza namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa, naishukuru familia yangu kwa kunitia moyo, nawashukuru wachezaji wenzangu kwa ushirikiano walionipa uwanjani na mashabiki walionipigia kura.
“Tuzo hii inaongeza hamasa kwa wachezaji ya kuipambania timu, kila mmoja anafanya jitihada za kuipata na hilo ni jambo zuri kwa timu, kwangu ni mara ya pili msimu huu kuichukua, lengo langu ni kuchukua tena na tena kwa kuwa mpira ndio kazi yangu na nipo hapa kuisaidia Simba,” alisema. Chama.
Chama ambaye ni kinara wa pasi zilizozaa mabao mpaka sasa akiwa amepiga 12, kwa tuzo ya Simba amevuna kiasi cha Sh 2,000,000 huku ile ya Ligi Kuu akijizolea kitita cha Sh 1,000,000.
Katika mwezi Desemba, Chama amecheza mechi tano ambapo alifunga mabao manne na kusaidia kupatikana kwa mengine saba kwa maana ya pasi za mwisho za mabao.
