Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ametamba kuifunga Simba katika mchezo wa Ligi Kuu NBC utakaochezwa Desemba 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema kinachompa matumaini ya kushinda mchezo huo ni wakati mgumu wanaopitia wapinzani wao Simba, kwenye michuano ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Simba ni timu yenye wachezaji wazuri hilo hatulipingi lakini kuhusu uzoefu hata Kagera Sugar tuna uzoefu wa kutosha, cha msingi tumejipanga kupata pointi tatu katika mchezo huo bila kujali tunacheza wapi na timu gani,” alisema Maxime.
Alisema hawapo tayari kupoteza mechi mbili mfululizo baada ya wiki iliyopita kufungwa na Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kagera Sugar inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 13 baada ya michezo 11 huku Simba ikishikilia nafasi ya tatu kwa pointi 19 baada ya mechi nane.
