Na mwandishi wetu
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kidao Wilfred ameeleza kusikitishwa kwake na madai yaliyotolewa na msemaji wa klabu Yanga aliyesimamishwa, Haji Manara aliyedai kuwa Kidao alimuomba msamaha kwa kuwa Rais wa TFF, Walace Karia alifanya makosa.
Taarifa ya TFF iliyopatikana hii leo na kusainiwa na ofisa habari na mawasiliano wa shirikisho hilo, Clifford Ndimbo ilimnukuu Kidao akisema kuwa maelezo hayo ya Manara si ya kweli na sekretarieti ya TFF haina muda wa kulizungumzia jambo ambalo limeshatolewa uamuzi na chombo huru cha TFF.
Sekretarieti ya TFF ilifungua shauri kwenye kamati ya maadili dhidi ya Manara baada ya kutokea mzozo kati yake na Karia kwenye jukwaa kuu la Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la FA kati ya Coastal Union na Yanga uliopigwa Julai 2 mwaka huu.
Sekretarieti ya TFF katika mashitaka yake kwenye kamati hiyo ilidai kuwa siku mzozo huo ulipotokea Manara alimshambulia Karia kwa maneno akimwambia: “Wewe unanifuatafuata sana na hii ni mara ya tatu, sikuogopi kwa lolote nina uwezo wa kukufanya lolote na huna uwezo wa kunifanya lolote.”
Katika utetezi wake wa awali, Manara alidai kuwa yeye si kichaa kwa hiyo hawezi kutamka maneno hayo mbele ya watu bila ya kuwa amechokozwa na hakukuwa na kutukanana zaidi ya kutofautiana kidogo kati yake na ndugu Karia.
Kamati ya maadili hata hivyo Julai 21 mwaka huu baada ya kusikiliza pande zote ilitangaza kumfungia Manara kutojihusisha na shughuli za mchezo wa mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kwa miaka miwili na kumtoza faini ya Sh milioni 20.
Kamati hiyo pia iliuarifu umma kuwa Manara na sekretarieti ya TFF wote wana haki ya kukata rufaa kama hawajaridhishwa na hukumu hiyo.
Soka Kauli ya Manara yamsikitisha Kidao
Kauli ya Manara yamsikitisha Kidao
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
