Nyon, Uswizi
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na rais wake, Gianni Infantino wamelaumiwa kwa usaliti kupitia barua ya wazi ya mashirikisho ya soka Ulaya (Uefa), Marekani Kusini (Concacaf) na Asia.
Barua hiyo ambayo imesainiwa marais na makatibu wakuu wa mashirikisho hayo matatu, imeeleza kuwa hoja ya hivi karibuni yenye utata inayohusisha Fifa Foward Enterprise (FFE) msingi wake ni kuhusu hadhi ya soka na hadhi ya waliochaguliwa kuongoza mchezo huo.
Kwa mantiki hiyo FFE ilitaka kuwe na taasisi mpya itakayoundwa kusimamia haki za kibiashara na mauzo ya tiketi katika mashindano yote yanayosimamiwa na Fifa zikiwamo fainali za Kombe la Dunia ambapo asilimia 21 ingeuzwa kwa kampuni binafsi.
Mpango huo ulivunjwa baada ya kuibuka shutuma kutoka mashirikisho ya soka yakiongozwa na Uefa, shirisho ambalo lilitishia kususia mashindano yote ya soka yanayoandaliwa na Fifa.
“Inapotokea uaminifu ukavunjwa kwa kufanyika ulaghai, pale mtu mmoja anapoamua kujiweka juu ya ushirika uliomuamini na kumpa madaraka, hapo uaminifu unakuwa umewekwa kando,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
“Uongozi wa soka si jambo analomiliki mtu, si suala linaloshikiliwa na mtu au kulazimisha kushika madaraka badala yake ni wajibu wa kuzihudumia mamlaka za familia ya soka ambazo zimekuamini,” ilieleza barua hiyo.
Barua hiyo hata hivyo haikumtaja moja kwa moja Rais wa Fifa, Gianni Infantino lakini kilichopo ni kwamba mlengwa mkuu wa hoja hizo ni kiongozi huyo ambaye ni kama vile anatakiwa ajiuzulu.
Barua ya mashirikisho hayo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Fifa kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari ikielezea kuhusu inachokiona kuwa ni juhudi za kififisha hadhi ya shirikisho hilo na Infantino.
