Na mwandishi wetu
Baada ya kutangazwa kikosi cha Taifa Stars, makocha wazawa wameonesha kuunga mkono kikosi hicho wakiamini Kocha Mkuu, Adel Amrouche ana mipango thabiti kuelekea mechi na Algeria.
Kocha wa zamani wa Stars, Charles Mkwasa amekipongeza kikosi hicho kwa kuwa na vijana wengi na baadhi ya wakongwe akiamini mchanganyiko wao utaleta matokeo chanya kwenye mechi hiyo ya kuwania kufuzu kushiriki Afcon.
“Nafikiri ni timu ya kawaida nzuri, ina vijana wengi na wakongwe wachache na kwa kuwa ni jukumu la kocha mwenyewe kuita kikosi kizuri siwezi kukosoa nikiamini wako sahihi namna walivyochagua naamini walitazama hata kikosi chao cha kwanza kitakuwaje,” alisema.
“Lakini mechi ni ngumu dhidi ya Algeria maana wapinzani wanafahamika na hawajafungwa mpaka sasa, nafikiri kwa nafasi waliyopo hawatakuja kucheza kwa presha na hiyo ni nafasi yetu ya kutumia njia ya kujilinda kwa kumiliki mpira muda mwingi na kama tukikosa ushindi basi tupate sare itatusaidia,” alisema Mkwasa.
Naye winga wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ alisema: “Kikosi kipo vizuri tu, sababu waliochagua ni wataalamu, wao ndio wenye kazi yao na hakuna anayechagua kikosi akafanye vibaya, hivyo tusiwavuruge kwa kutaka wachezaji tunaowapenda sisi binafsi ndio waitwe.
“Mfano mtu anasema Fei (Feisal Salum) ameachwa lakini wao si wataalamu wa kufahamu Fei amekosa nini wakati ligi inamalizika na yeye yupo nje kabla ya kuanza kucheza tena hivi karibuni, wakumbuke Stars sio ya mtu mmoja, na wengine waitwe ili kuwe na mzunguko mzuri wa utengenezaji wa timu,” alisema SMG.
Naye kocha wa zamani wa Mbeya City, Yanga na Azam, Juma Mwambusi alisema yeye anaunga mkono uteuzi wa kikosi hicho kwani anaamini kila kocha ana falsafa yake ndicho kinachomwongoza katika kuita kikosi hivyo yeye anaamini Amrouche atawapa kitu kupitia kikosi hicho.
Fred Minziro ambaye ni kocha wa Tanzania Prisons alieleza kwa kifupi kuwa anaheshimu mchango wa kocha huyo Stars na angependa asimuingilie kwenye kazi yake zaidi ya kuunga mkono kile anachokifanya kwa faida ya taifa.
Beki wa zamani wa Yanga na Simba, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ alisema: “Kwangu naona ni timu waliyojaribu kuchagua wazoefu na vijana, nadhani chaguo la safari hii ni chaguo zuri sana, Watanzania tusikariri kuhusu kuitwa kwa wachezaji fulani kwa ulazima, mpira ni mchezo wa muda na umri, tuwape nafasi wengine pia.”