Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema wachezaji wapya waliotua kwenye kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa 2022/23 wameongeza ushindani wa namba na ari kwenye kikosi chake.
Nabi amezungumza hayo kutokana na matokeo ya maandalizi ya siku nne pekee za awali za maandalizi ya msimu ujao yanayoendelea huko Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu ya NBC na Kombe la FA, wapo kwenye maandalizi hayo wakiwa na wachezaji wao wapya waliowatambulisha mpaka sasa kasoro Bernard Morrison ambaye anatarajia kuanza rasmi mazoezi keshokutwa Alhamisi.
Wachezaji wapya walioanza mazoezi na timu hiyo ni Stephane Aziz Ki, Joyce Lomalisa, Lazarous Kambole na Gael Bigirimana ambao wametajwa kutua Yanga kutokana kazi kubwa waliyoonyesha kwenye timu walizotoka.
Nabi ameelezea namna nyota hao walivyonogesha maandalizi yao kutokana na upambanaji na uwezo wanaouonyesha mpaka sasa.
“Kila mchezaji ameonyesha kutaka kudhihirisha kitu na kuipigania timu kwa ajili ya kuthibitisha thamani yake kwangu, najisikia furaha kufundisha timu ya namna hii kwani ushindani utakuwa mkubwa na hatutakuwa na wachezaji wazembe, hilo ni jambo zuri kutokana na malengo yetu kwa msimu ujao,” alisema Nabi.
Kocha huyo ameeleza kuwa mipango yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi katika mashindano yote watakayoshiriki na kwa namna walivyoanza anaamini walichokusudia kinaweza kutokea kama ari hiyo waliyoanza nayo itaendelea kwa msimu mzima.
Soka Nabi awafurahia mastaa wapya
Nabi awafurahia mastaa wapya
Read also