Na mwandishi wetu
Timu ya Mashujaa imeanza kuimarisha kikosi chao baada ya kukamilisha usajili wa wachezaji watatu katika dirisha hili la usajili tangu lilipofunguliwa Desemba, mwaka jana.
Nyota ambao hadi sasa wamemwaga wino wa kuitumikia Mashujaa ni Nyenyezi Juma kutoka Inter Stars ya Ligi Kuu Burundi, Balama Mapinduzi mchezaji huru baada ya kuachana na Coastal Union na Emmanuel Mtumbuka kutoka Stand United.
Akizungumza na GreenSports, kocha mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ alisema kuwa lengo la kufanya sajili hizo ni kuimarisha kikosi chao ambacho kipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.
“Tunataka kutumia dirisha hili la usajili kujiimarisha, hatuko kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hivyo tunapaswa kubadilika na wakati ndio huu ligi kuu ikiwa imesimama.
“Kuna baadhi ya wachezaji tunaenda kuachana nao kwenye kipindi hiki na kuleta nyota wapya ambao watakuja kuleta kitu kipya na kutuondoa mahali tulipo hivi sasa,” alisema Baresi.