Munich, Ujerumani
Kocha wa Bayern Munich ambaye tayari amefikia makubaliano ya kuachana na timu hiyo baada ya msimu huu, Thomas Tuchel amesema pamoja na makubaliano hayo lakini lolote linawezekana.
Mapema Feberuari mwaka huu klabu ya Bayern ilitangaza kuwa Tuchel ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 50 ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu baada ya makubaliano ya pande zote mbili.
Uamuzi wa Bayern umetokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga ambapo timu hiyo iliyokuwa ikiwania kulibeba taji hilo kwa mara ya 12 mfululizo imeshindwa kufanya hivyo.
Badala yake Bayer Leverkusen imeibuka kuwa tishio kwenye ligi hiyo na tayari imeshatawazwa kuwa bingwa mpya wa taji hilo na kuiacha Bayern na rekodi yake ya kubeba taji la ligi hiyo kwa misimu 11 mfululizo.
Mambo hata hivyo yako tofauti kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo timu hiyo imefuzu hatua ya nusu fainali na katika mechi ya kwanza dhidi ya Real Madrid imefanikiwa kutoka sare ya mabao 2-2.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuendelea kuwa na timu hiyo Tuchel alisema kwamba hayo ni makubaliano ambayo hayawezi kubadilika lakini hapo hapo akasema kwamba lolote linawezekana.
“Ni kweli kwamba unaweza kubadili mkataba wowote kwa makubaliano, na hapa tuna mkataba ambao tulikubaliana kuumaliza mapema, lakini katika mkataba huo pia lolote linawezekana,” alisema Tuchel.
Taarifa nyingine hata hivyo zinadai kwamba Tuchel anajiandaa kuachana na timu hiyo na hesabu zake zipo katika klabu ya Man United ambayo kocha wake, Erik ten Hag naye anapitia wakati mgumu.