Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa Simba, Daniel Cadena, amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao aliyoaindaa vyema kutafuta ushindi itakapokuwa inacheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas.
Cadena ameeleza hayo Ijumaa hii alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
“Ni muhimu kubadili kilichopita, nina furaha na kiwango cha wachezaji wangu tumetoka kubadili benchi la ufundi kila kitu kinabadilika lakini tumejipanga kupata ushindi.
“Tunaenda kucheza na timu nzuri lakini kama kocha kazi yangu ni kuandaa timu yangu ili ipate ushindi kwenye mchezo huu muhimu,” alisema Cadena.
Alisema kuwa katika mchezo huo watawakosa Aishi Manula ambaye amepata maumivu na Clatous Chama ambaye watamuangalia kwanza kabla ya kumjumuisha katika mechi hiyo kutokana na kuchelewa kujiunga na timu akitokea kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Zambia.
“Tunafahamu juu ya kumkosa mchezaji muhimu kikosini, kama benchi tumejipanga juu ya hilo maana unapomkosa mchezaji mkubwa unapaswa kuwa na mpango zaidi zaidi ya mmoja.
“Kingine ni hamasa ya wachezaji iko chini, mashabiki wasiniache peke yangu nawaomba mashabiki waje kwa wingi kuwapa sapoti wachezaji katika mchezo huu muhimu,” alisema Cadena.
Kocha mkuu wa Asec Mimosas, Julien Chevalier, alisema ana furaha kuwa kwenye Ligi ya Mabingwa kwani ni mashindano muhimu na wanapaswa kushinda ili kusogea hatua inayofuata.
“Tutacheza jinsi ambavyo Simba wataingia, waandishi wengi wanapenda kuniuliza kuhusu mchezo niliopoteza kwenye Uwanja wa Mkapa, hilo sisi hatuangalii tunachoangalia mchezo wa kesho.
“Ligi ya Mabingwa Afrika ni mashindano makubwa na muhimu hivi sasa tuna uzoefu wa kutosha na tupo tayari kukabiliana na Simba.
“Tuko tayari kuendeleza rekodi yetu kwenye mashindano makubwa, hatuangalii kilichotokea kwenye mashindano makubwa mwaka 2022, timu zilipitia vipindi vigumu ikiwemo Covid 19 lakini sasa hali ni tofauti,” alisema Chevalier.
Timu hizo za Kundi B katika michuano hiyo, zinakutana mara ya tatu sasa ambapo ziliwahi kukutana mara mbili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2022.
Katika mchezo wa kwanza Simba ilishinda kwa mabao 3-1 kabla ya Asec nayo kushinda ikiwa nyumbani kwa mabao 3-0.