Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeisifu Azam FC kwa uungwana iliouonesha kwenye suala la usajili wa kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwa kufuata taratibu na kumaliza usajili wa mchezaji huyo kwa weledi.
Kauli hiyo imetolewa baada ya kukamilika kwa dili la mchezaji huyo kuhamia Azam akitokea Yanga baada ya msuguano wa takriban miezi sita, mchezaji huyo akishinikiza kuvunja mkataba wake na Yanga kutokana na sababu za kimaslahi na nyinginezo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Yanga, Ally Kamwe alisema kuwa Azam walifuata chaguo namba tatu la Yanga la timu inayomuhitaji Fei kwenda kuzungumza na Yanga, kitu ambacho Azam wamekifanya na kumaliza salama.
“Kama unakumbuka baada ya maamuzi ya kamati (Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF) tukatoa machaguo matatu na mojawapo la klabu inayomuhitaji Fei kuja kuzungumza nasi na Azam ikafanya hivyo.
“Kwa hiyo Azam wamekuwa waungwana kwa kuja kugonga hodi na kuulizia bei ya Feisal waweze kumnunua, hivyo tunashukuru Azam wamekuja mbele wao wakasema wako tayari, ni jambo la kiungwana na ndivyo mpira ulivyo na klabu tumeimaliza biashara hiyo tukimtakia Fei kila la heri,” alisema Kamwe.
Fei ambaye amekabidhiwa jezi namba sita Azam aliyokuwa akiitumia alipokuwa Yanga, anaihama Yanga baada ya kudumu kwa msimu mitano tangu alipojiunga akitokea JKU ya Zanzibar mwaka 2018.
Soka Yanga: Azam waungwana
Yanga: Azam waungwana
Read also