Na mwandishi wetu
Simba hatimaye imefufua matumaini yake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupata ushindi wa ugenini wa bao 1-0 dhidi ya Vipers ya Uganda Jumamosi hii.
Bao hilo pekee la Simba lililopatikana dakika ya 20 lilifungwa na Henock Inonga baada ya pasi nzuri ya kichwa kutoka kwa Moses Phiri ambaye kwa muda mrefu alikuwa majeruhi.
Kocha wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho ambaye aliwahi kuinoa Vipers kabla ya Simba, aliwapanga eneo la ushambuliaji Saido Ntibazonkiza, Moses Phiri, Kibu Denis na Clatous Chama.
Mbinu ya kocha huyo pengine ilikuwa na lengo la kushambulia sana lango la Vipers na kupata mabao lakini mwisho wa siku, Simba ilitoka na bao hilo pekee la Inonga.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi tatu na kushika nafasi ya tatu wakati Vipers imerudi mkiani ikiwa haina pointi hata moja. Vinara wa kundi hilo ni Raja Casablanca na Horoya ya Guinea inashika nafasi ya pili.
Simba ambayo ilianza kupoteza matumaini ya kusonga mbele katika michuano hiyo baada ya kupoteza mechi mbili za awali dhidi ya Horoya na Raja sasa ina kila sababu ya kujivunia kwa kufufua matumaini.
Timu hiyo hata hivyo bado ina kazi ya kupigania matokeo katika mechi tatu zilizobaki ili kujihakikishia kusonga mbele kwa kufikisha walau pointi saba na hivyo kumaliza mechi za kundi lake na pointi 10.
Simba sasa inasubiri kucheza mechi mbili za nyumbani dhidi ya Vipers na Horoya na moja ya ugenini dhidi ya Raja, mechi ambazo zinashikilia hatma ya timu hiyo kusonga mbele hatua ya robo fainali.
Simba hata hivyo itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutumia nafasi kadhaa ambazo zingeweza kuipa timu hiyo ushindi lakini umaliziaji ulibaki kuwa tatizo kwa timu hiyo.
Mfano mmojawapo ni dakika ya 85, Clatous Chama aliunasa mpira katikati ya uwanja na kumtoka beki mmoja wa Vipers lakini wakati akielekea kwenye lango la timu hiyo alizidiwa mbio na beki mwingine wa Vipers hatimaye akapiga shuti dhaifu la ‘kujitoa lawama’.
Chama hata hivyo alionekana kuchechemea baada ya shambulizi hilo kabla ya kutolewa nje ya uwanja akiwa amebebwa na baadaye kufanyiwa mabadiliko na nafasi yake kuingia Kennedy Juma.
Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Zimbwe Jr, Joash Onyango, Inonga, Kanoute, Kibu Denis/Habib Kyombo, Muzamir, Phiri/Nyoni, Ntibazonkiza, Chama/Kennedy Juma.
Kimataifa Simba yafufua matumaini Afrika
Simba yafufua matumaini Afrika
Read also